Doha, Qatar
Nyota wa zamani wa Senegal, El Hadji Diouf amemtaka mshambuliaji Sadio Mane kutulia na kukabiliana na ugumu wa kuzikosa fainali za Kombe la Dunia zitakazoanza kesho Jumapili.
Mane, mmoja wa wachezaji muhimu wa Senegal, hatokuwamo kwenye kikosi cha Senegal baada ya kuumia mguu wakati akiiwakilisha Bayern Munich kwenye mechi ya Bundesliga dhidi ya Werder Bremen na kutoka uwanjani baada ya dakika 20.
“Sote tuna huzuni kwa sababu tungependa kumuona akicheza kwenye fainali za Kombe la Dunia na kwa sababu Sadio mwenyewe alifanya kila kitu ili awe tayari kwa ajili ya Kombe la Dunia,” alisema Diouf mwanasoka bora wa mwaka wa Afrika mara mbili.
“Wachezaji wote wakubwa wanataka kutamba kwenye fainali za Kombe la Dunia, lakini kuna mambo ambayo yanaweza kutokea, tunakwenda kucheza bila ya uwapo wake na tunakwenda kufanya kila kitu ili kumfanya awe na cha kujivunia, nafikiri Sadio atakuwa imara atakaporudi kwa mara nyingine,” alisema Diouf.
Diouf ambaye alikuwa kwenye kikosi cha Senegal kilichoshiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka 2002 na kufikia hatua ya robo fainali, bado ana imani kubwa kwamba Senegal itaweza kufuzu na kucheza hatua ya mtoano.
“Huwa nazungumza na Mane kila mara, najua kuna timu ambazo hazitaki kucheza na Senegal kwa sababu tuna timu nzuri yenye wachezaji wazoefu,” alisema Diouf, nyota wa zamani wa Liverpool ambaye kwa sasa yuko Qatar na timu ya Senegal.
Rais wa Senegal, Macky Sall naye ni miongoni wa watu ambao wametuma salamu za pole kwa Mane kupitia mitandao ya kijamii.
Senegal ambao ni mabingwa wa Afrika watacheza mechi yao ya kwanza ya Kundi A dhidi ya Uholanzi keshokutwa Jumatatu kabla ya kuumana na wenyeji Qatar Novemba 25 na kumalizia mechi yake ya mwisho ya makundi dhidi ya Ecuador, Novemba 29.
Kimataifa Diouf amtuliza Sadio Mane
Diouf amtuliza Sadio Mane
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
