Na mwandishi wetu
Azam FC imeichapa Dodoma Jiji mabao 3-1 na kuchupa hadi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu NBC baada ya kufikisha pointi 30 katika mechi 13 ilizocheza hadi sasa.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, wenyeji Dodoma Jiji ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya saba baada ya Yanick Bangala kujifunga.
Iliwachukua dakika nne, Azam kusawazisha bao hilo kupitia kwa Nassor Saaduni na kuongeza bao la pili muda mfupi kabla ya timu kwenda mapumziko kwa bao la penalti lililofungwa na Feisal Salum au Fei Toto.
Kama ilivyokuwa kwa Azam, Dodoma Jiji nao waliwazawadia Azam bao la bure baada ya nyota wake Dickson Mhilu kujifunga katika dakika ya 60.
Azam pamoja na ushindi huo kuwawezesha kushika usukani lakini wanafuatiwa kwa karibu na Simba wanaoshika nafasi ya pili wakiwa na pointi 28 na Yanga wanaoshika nafasi ya tatu na pointi zao 27.
Simba na Yanga pia zimecheza mechi 11 hadi sasa wakati Azam imecheza mechi 13 hivyo timu hiyo inaweza kushushwa kileleni wakati wowote vinginevyo iendelee kushinda huku ikiziombea Simba na Yanga zipoteze mechi zao.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa Jumapili, bao pekee la George Mpole liliiwezesha Pamba Jiji kutoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ken Gold.
Mechi kati ya Coastal Union na Prisons ilishindwa kuchezwa baada ya Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha kujaa maji kutokana na mvua na mechi hiyo sasa inachezwa Jumatatu.
Soka Azam yashika usukani ligi kuu
Azam yashika usukani ligi kuu
Read also
