Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa KMC, Abdihamid Moallin (pichani) amesema mwenendo mzuri walionao kwenye Ligi Kuu NBC msimu huu unampa matumaini ya kufikia malengo yao waliyojiwekea.
Timu hiyo inashika nafasi ya tatu ikikusanya pointi 15 katika michezo minane iliyocheza tangu kuanza kwa msimu huu.
Akizungumza na GreenSports, kocha huyo alisema ushirikiano uliopo ndiyo siri kubwa ya matokeo mazuri wanayoyapata katika mechi zao.
“Naupongeza uongozi, wamekuwa mstari wa mbele katika kutimiza majukumu yao na wachezaji nao wamekuwa wakijituma kwa kutoa jasho lao lote kuhakikisha timu inapata ushindi,” alisema Moallin.
Kocha huyo alisema pamoja na kuwa katika nafasi nzuri lakini bado wanakazi kubwa kuhakikisha wanamaliza msimu kwenye nafasi za juu ili kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa ambayo wamepanga kushiriki msimu ujao.
Alisema mpango wao wa awamu ya kwanza ni kuhakikisha wanamaliza mzunguko wa kwanza kwenye ndani ya nne bora ili mzunguko wa pili wawe na kazi rahisi ya kufikia lengo lao.
KMC ni miongoni mwa timu ambazo zilinusurika kushuka daraja msimu uliopita kabla ya kuangukia kwenye mechi za mtoano na kuifunga Mbeya City na kujinusuru kabla ya msimu huu kufanya usajili mzuri ikiwemo kubadili benchi la ufundi na kumleta Moallin ambaye ameiimarisha timu hiyo.