Na Hassan Kingu
Kamati ya Rufaa ya Maadili ya TFF imempunguzia faini msemaji wa Yanga, Haji Manara kutoka Sh milioni 20 hadi milioni 10, lakini adhabu ya msingi na inayomtesa ya kumtenga na familia ya soka kwa miaka miwili iko pale pale…
Kwa maana nyingine kamati imempunguzia adhabu ambayo haikuwa ikimshughulisha sana, ile adhabu inayomnyima raha na kumsumbua kichwa imeachwa vile vile, kwa hiyo Manara anaendelea kupata maumivu ya adhabu kwa kuwa kilichopunguzwa si kile ambacho kilikuwa kikimtesa sana.
Kamati hata ingeamua kumuongezea faini hadi Sh milioni 25, Manara asingeumia, Yanga wanaomkubali wasingeshindwa kuchangishana au uongozi usingeshindwa kulifanyika kazi jambo hilo na kulimaliza na Manara kuruhusiwa kuendelea na shughuli za soka kama kawaida.
Kilichofanywa na kamati ni kama vile kupoza tatizo dogo wakati tatizo kubwa na la msingi lipo vile vile, ni sawasawa na mgonjwa aliyepewa dawa za usingizi akalala na baada ya kuamka maradhi yake anayakuta yako vile vile. Ndicho alichofanyiwa Manara, tatizo au maradhi yaliyomfanya akate rufaa hayajashughulikiwa na ‘daktari’ hata kidogo.
Badala yake alichofanya daktari ni kuhangaika na tatizo dogo ambalo hata angeliacha mgonjwa asingelalamika, ni tatizo ambalo mgonjwa anamudu kukabiliana, lipo ndani ya uwezo wake lakini daktari kachagua kujishughulisha kulipunguza. Daktari hajamsaidia mgonjwa, amempunguzia mzigo mdogo ambao mgonjwa anauweza akamuacha apambane na mzigo mzito unaomtesa.
Uamuzi wa kukata rufaa ilikuwa ni hatua muhimu ya kujikwamua na adhabu kubwa, kutaka ipunguzwe au ifutwe, matarajio hayo yametoweka pale adhabu hiyo inapoachwa vile vile badala yake ile adhabu isiyoumiza ndiyo inayopunguzwa. Kwa Manara hapa kamati imemuachia maumivu yale yale na kimsingi adhabu yake iko pale pale.
Achana na Manara, kumtenga mtu yeyote wa soka na familia ya soka kwa miaka miwili si jambo dogo hasa kwa mtu ambaye amekulia katika familia hiyo na amejiaminisha katika kuyatumikia maisha yanayohusisha soka, mchezo unaopendwa na wengi, ni wazi kwamba miaka miwili ni mingi mno kwa mtu huyo kujitenga na familia hiyo.
Kitu pekee kilichobaki kwa Manara kwa sasa ni kutafuta namna ya kulimaliza suala hili kwa namna nyingine, iwe ni kuwahusisha viongozi wa juu wa TFF, waziri na watu wengine ambao wanaweza kutoa ushawishi kwa mamlaka za TFF kumpunguzia mzigo wa adhabu inayomtesa au kuufuta.
Vinginevyo tuache kudanganyana kwamba miaka miwili ni michache au Manara haumii kwa kufungiwa miaka miwili, ni kweli miaka miwili itakuja na kuondoka na kuja mingine lakini ukweli unabaki pale pale kwamba miaka miwili ni mingi na inamtesa Manara.
Manara alijikuta katika adhabu hiyo baada ya kudaiwa kumtamkia maneno yasiyofaa Rais wa TFF, Walace Karia, kosa ambalo anadaiwa kulifanya Julai 2 mwaka huu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha wakati wa mechi ya fainali ya Kombe la FA kati ya Yanga na Coastal Union.
Soka Kimsingi adhabu ya Manara iko pale pale
Kimsingi adhabu ya Manara iko pale pale
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
