Na mwandishi wetu
Wachezaji wa timu za Dodoma Jiji, Augustino Nsata na Edson Katanga wa JKT Tanzania wamefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya Sh milioni moja kwa kila mmoja kwa kosa la kupigana uwanjani.
Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika taarifa yake ya Jumamosi Juni 27, 2026 ilieleza kuwa wachezaji hao walipigana katika mechi ya ligi kuu baina ya timu hizo iliyoisha kwa sare ya bila kufungana.
Timu nyingine zilizoadhibiwa na kamati hiyo ni Tanzania Prisons iliyotozwa faini ya Sh milioni tano kwa kosa la wachezaji wake kujihusisha na vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina.
Katika mechi yao dhidi ya JKT Tanzania iliyoisha kwa Prisons kupata ushindi wa bao 1-0, wachezaji hao walionekana wakimwaga vitu mbalimbali walivyokuwa navyo mkononi kabla ya kujikusanya katikati na kupasua mayai.
Prisons pia imepewa onyo kali kwa kuchelewa kufika uwanjani katika mechi hiyo, ambapo badala ya kufika saa 8:30 mchana, timu hiyo ilifika saa 8:40 jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya mchezo husika.
Nayo timu ya Mashujaa imetozwa faini ya Sh milioni tano kwa kosa la wachezaji wake kujihusisha na matukio yanayoashiria imani za kishirikina kabla ya mchezo wao na Fountain Gate.
Mashujaa ambao katika mchezo huo walitoka na ushindi wa bao 1-0, wachezaji wake walionekana kabla ya mechi wakimwaga uwanjani vitu vyenye asili ya vimiminika.
Katika Ligi ya Championship, meneja wa timu ya Gunners, Karim Rashid ametozwa faini ya Sh milioni moja kwa kosa la kuwatukana waamuzi na kamisaa wa mchezo wao dhidi ya Polisi Tanzania.
Mchezo huo ambao uliisha kwa Polisi Tanzania kutoka na ushindi wa mabao 2-1, mara baada ya dakika 90 kumalizika, meneja huyo alionekana akimtukana mwamuzi na baadaye kamisaa.
Katika hatua nyingine klabu ya Mapinduzi ya mkoani Mwanza imeadhibiwa kwa kushinda kufika kwenye Uwanja wa TFF Centre, Dar es Salaam kwa ajili ya mechi yao ya Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Magnet FC.
Kwa kosa hilo Mapinduzi inakuwa imepoteza hadhi ya kuingia hatua inayofuata (kusalia kwenye ligi hiyo).
Klabu hiyo pia imetozwa faini ya Sh milioni mbili na kutakiwa kulipa fidia ya maandalizi ya mchezo huo huku mwenyekiti wa klabu hiyo, Baraka Kitaya Munanga akifungiwa kujihusisha na soka kwa miezi 12.
Kimataifa Klabu zaadhibiwa kwa ushirikina, wachezaji kupigana
Klabu zaadhibiwa kwa ushirikina, wachezaji kupigana
Read also
