Na mwandishi wetu
Aliyekuwa kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi ni miongoni mwa makocha waliowasilisha CV zao kuomba kazi ya kuinoa timu ya Raja Casablanca ya nchini Morocco.
Raja, moja ya timu zenye jina kubwa barani Afrika kwa zaidi ya wiki moja sasa imekuwa bila ya kocha tangu ichukue uamuzi wa kuachana na aliyekuwa kocha wao mkuu, Ricardo Pinto.
Gamondi amekuwa akitajwa zaidi kwa sababu ni kati ya makocha wenye uzoefu na soka la nchini Morocco kwani hapo kabla amewahi kuwa mkurugenzi wa ufundi wa klabu ya Waydad Casablanca ambao ni mahasimu wa Raja.
Rais wa klabu ya Raja, Adel Halla alinukuliwa na chanzo kimoja cha habari hivi karibuni akisema kwamba hawana haraka ya kumpata mrithi wa Pinto na kukiri kwamba wana majina mengi mezani.
“Tutatumia muda wa kutosha katika kuuchagua jina sahihi ambalo litaendana na malengo na matakwa ya timu,” alisema Halla.
Gamondi ambaye ni raia wa Argentina kwa sasa hana timu tangu kuachana na Yanga Novemba mwaka jana na hivi karibuni zimekuwapo habari kwamba kocha huyo ni kati ya makocha wanaopewa nafasi kubwa ya kukabidhiwa jukumu la kuinoa Raja.
Miongoni mwa mafanikio ya Gamondi akiwa na Yanga mbali na kutwaa taji la Ligi Kuu NBC lakini pia aliifikisha timu hiyo robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Raja inashika mkia katika kundi lake ikiwa haijashinda hata mechi moja na hiyo inatajwa kuwa sababu mojawapo ya kutimuliwa kwa Pinto.
