London, England
Klabu ya Tottenham Hotspur imeyataka makampuni ya mitandao ya kijamii kuchukua hatua baada ya mchezaji wao, Son Heung-min kushambuliwa kwa kutolewa maneno ya dhihaka za ubaguzi wa rangi.
Son, nyota kutoka Kora Kusini alikutana na dhihaka hizo baada ya Spurs kutoka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya West Ham huku mchezaji huyo aliyeingia akitokea benchi akiwa mfungaji wa bao la pili.
Spurs walitoa taarfa kupitia akaunti yao ya Twitter wakidai kuwasilisha malalamiko kuhusu dhihaka alizofanyiwa Son. “Tuko pamoja na Son, tunayataka makampuni ya mitandao ya kijamii na mamlaka kuchukua hatua.”
“Tumepata taarifa kuhusu kauli za dhihaka za kibaguzi kwenye mitandao ya kijamii zikielekewa kwa Heung-Min Son wakati wa mechi ya leo (jana Jumapili),” ilifafanua taarifa ya klabu hiyo.
Kikundi maarufu kinachopiga vita ubaguzi wa rangi cha Kick It Out, mapema mwezi huu kilitoa taarifa ya kutaka mabadiliko ya msingi yafanyike baada ya mshambuliaji wa Brentford, Ivan Toney kukumbana na kadhia ya ubaguzi wa rangi kwenye mtandao wa Instagram.
Toney alijikuta katika kadhia hiyo baada ya kufunga bao la kusawazisha katika mechi na Arsenal, bao ambalo liliibua utata ikielezwa kwamba lilitakiwa kukataliwa kwa mujibu wa picha za VAR kwa kuwa mchezaji mwenzake Christian Norgaard alikuwa ameotea.
Oktoba mwaka jana Norgaard alisema kwamba alishambuliwa kwa maneno ya dhihaka za kibaguzi kwenye mtandao wa Instagram baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Brighton.
Meta ambayo ni kampuni mama ya Instagram na Facebook na Instagram ililaani dhihaka dhidi ya mchezaji huyo lakini wakadai wasingeweza kuchukua hatua kwa sababu ujumbe huo haukuwasilishwa moja kwa moja kupitia ‘app’ yao.
Shabiki Antonio Neill mwenye umri wa miaka 24, baada ya uchunguzi wa polisi, mapema mwaka huu katika Mahakama ya Newcastle, alikiri kutuma ujumbe wa kumshambulia Toney.