Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imetangazwa kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania kipengele cha Klabu Bora kwa Wanaume Afrika katika tuzo zitakazotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) Desemba 11, mwaka huu.
Taarifa hiyo imetangazwa leo Jumatano na Mtandao wa Caf juu ya tuzo hizo zinazotarajiwa kufanyika jijini Marrakesh, Morocco.
Katika kinyang’anyiro hicho, Yanga itachuana na klabu za CR Belouizdad, USM Alger za Algeria, Asec Mimosas ya Ivory Coast, Al Ahly ya Misri, Raja Casablanca, Wydad AC za Morocco, Mamelodi Sundowns, Marumo Gallants za Afrika Kusini na ES Tunis ya Tunisia.
Miongoni mwa yaliyosababisha miamba hiyo ya soka nchini kupenya kwenye kinyang’anyiro hicho ni mafanikio makubwa waliyoyapata katika misimu miwili iliyopita katika michuano ya ndani na ya klabu Afrika.
Yanga imekuwa bingwa wa Ligi Kuu NBC kwa misimu miwili mfululizo ikiwemo kutwaa ubingwa wa Kombe la FA (ASFC) mara mbili mfululizo na msimu uliopita ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kipa wa timu hiyo, Djigui Diarra raia wa Mali anawania kipengele cha Mchezaji Bora wa Afrika pamoja na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Fiston Mayele ambaye kwa sasa anakipiga Pyramids ya Misri.
Pia Diarra anawania Tuzo ya Kipa Bora dhidi ya Mohamed El Shenawy (Misri), Yassine Bounou (Morocco), Andre Onana (Cameroon), Ronwen Williams (Afrika Kusini), Oussama Benbot (Algeria), Youssef El Motie (Morocco) na Edouard Mendy, Pape Mamadou, Landing Badji wote kutoka Senegal.
Rais wa Yanga, Hersi Saidi alisema kitendo cha Yanga kuingizwa kwenye kinyang’anyiro hicho ni heshima kubwa kwao na soka la Tanzania na hiyo ni kutokana na uwekezaji mkubwa ambao wameufanya katika misimu miwili iliyopita.
“Tunajivunia kuona Caf wanatambua uwepo wa Yanga katika soka la Afrika, unajua ni muda mrefu klabu hii ilipotea kwenye soka la ushindani na imepita miaka 25 kurudi kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, msimu uliopita tulicheza fainali ya Kombe la Shirikisho, kwetu ni mafanikio makubwa bila kujali kama tutashinda au tutakosa,” alisema Hersi.
Mbali na Yanga, timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ nayo imetajwa kwenye tuzo hizo ikiwania kipengele cha timu bora ya Taifa dhidi ya mataifa ya Morocco, Senegal, Cape Verde, Gambia, Guinea Bissau, Guinea ya Ikweta, Mauritania, Namibia na Msumbiji.