Jalisco, Mexico
Timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ‘DR Congo’ imefuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 mbele ya Jamaica na hivyo kurudi katika fainali hizo walizoshiriki mara ya mwisho miaka 52 iliyopita.
DR Congo ilipambana na Jamaica katika mechi hiyo ya play-off iliyochezwa Jumanne Machi 31, 2026 kwenye dimba la Akron nchini Mexico na kumalizika kwa sare ya bila kufungana katika dakika 90 kabla ya beki Axel Tuanzebe kufunga bao pekee katika dakika za nyongeza.
Ushindi huo umelihakikishia taifa hilo kushiriki fainali hizo zitakazoanza Juni 11, 2026 katika nchi za Canada, Mexico na Marekani na hivyo kujikumbusha walipofuzu mara ya mwisho mwaka 1974 wakati nchi hiyo ikiitwa Zaire chini ya Rais Mobutu Seseseko.
Mechi ya DR Congo ‘The Leopards’ na Jamaica ‘The Reggae Boyz’ kwa kipindi kirefu ilionesha kuwa na nguvu sawa kwa kila timu kutengeneza mashambulizi na umakini katika kujihami.
Hatimaye DR Congo walinufaika na shambulizi walilolifanya katika dakika ya 100 ambapo Tuanzebe aliruka juu kuuwahi mpira wa kona na kuujaza wavuni kwa kichwa hali iliyoamsha shangwe kwa mashabiki wake.
Kwa kufuzu huko, DR Congo inaingia katika fainali hizo ikiwa Kundi K ambalo pia lina timu za Colombia, Ureno na Uzbekistan.
DR Congo inaungana na timu nyingine tisa za Afrika kushiriki michuano hiyo na hivyo kufanya idadi ya timu za Afrika katika fainali za mwaka huu kuwa 10.
Timu nyingine za Afrika zilizofuzu kushiriki fainali hizo ni Misri, Algeria, Afrika Kusini, Senegal, Cape Verde, Morocco, Ghana, Tunisia na Ivory Coast.
Italia yakwama tena
Wakati mashabiki DR Congo wakishangilia kurudi kwenye fainali hizo baada ya miaka 52, nchini Italia ni huzuni baada ya timu hiyo mabingwa mara nne wa Kombe la Dunia kushindwa kufuzu kwa mara ya tatu mfululizo.
Italia ilishindwa kufuzu katika fainali hizo mwaka 2018 nchini Ufaransa na baada ya hapo ikashindwa kwa mara nyingine kufuzu katika fainali za Qatar mwaka 2022.
Kilichoiangusha Italia hadi kukosa fainali za 2026 ni mikwaju ya penalti katika mechi yao ya play-off dhidi ya Bosnia-Herzegovina iliyochezwa Jumanne Machi 31, 2026 na kumalizika kwa sare ya bao 1-1 katika dakika 90 za kawaida na 30 za nyongeza.
Italia chini ya kocha Gennaro Gattuso, kiungo aliyekuwa na timu ya Italia iliyobeba Kombe la Dunia mwaka 2006 nchini Ujerumani, ilishindwa kuonesha umahiri kwenye penalti baada ya kulala kwa penalti 4-1.
Bosnia-Herzegovina chini ya nahodha wake mkongwe Edin Dzeko, 40, kama DR Congo nayo inafuzu kwa mara ya pili katika historia ya nchi hiyo na imepangwa Kundi B na timu za Uswisi, Canada na Qatar.
Kimataifa DR Congo yafuzu Kombe la Dunia baada ya miaka 52
DR Congo yafuzu Kombe la Dunia baada ya miaka 52
Read also
