London, England
Arsenal jana jioni ililala kwa mabao 3-0 mbele ya Tottenham, kipigo kilichomkera kocha wa timu hiyo, Mikel Arteta ambaye amewashutumu waamuzi akidai wanauharibu mchezo mzuri wa soka.
Arteta ambaye timu yake imefungwa na kumaliza mchezo ikiwa na wachezaji 10 uwanjani, hata hivyo amekuwa makini katika kuwashutumu waamuzi hao huku akijihami kuwa anaweza kujikuta akifungiwa miezi sita kwa kusema ukweli.
“Kama nikisema ninachofikiria nitajikuta nafungiwa kwa miezi sita. Sijui namna ya kuongopa, kwa hiyo naamua kutosema kile ninachokifikiria, siwezi kusema ninachofikiria.”
Matokeo hayo yameathiri mbio za Arsenal katika kuwania nafasi ya nne bora kwenye Ligi Kuu England kwani licha ya kubaki nafasi ya nne ikiwa na pointi 66, Totenham inayoshika nafasi ya tano ina pointi 65 ikiwa ni tofauti ya pointi moja wakati kabla ya mechi ya jana Arsenal ilikuwa juu kwa tofauti ya pointi nne na sasa lolote linaweza kutokea katika mechi mbili zilizobaki za ligi hiyo.
Arsenal ililala kwa bao la penalti mfungaji akiwa ni Harry Kane, penalti iliyotolewa dakika ya 22 baada ya Heung-Min Son, staa kutoka Korea Kusini kuchezewa rafu na Cedric Soares.
Kane aliongeza bao la pili dakika ya 37 kwa penalti tena ambayo ilitolewa baada ya Heung-Min Son kuchezewa rafu, safari hii mhusika akiwa ni Rob Holding, kosa ambalo halikuishia kuzaa penalti tu bali Rob naye alilimwa kadi ya njano ikiwa ni ya pili na hivyo kupewa nyekundu na kutoka nje.
Alikuwa ni Heung-Min Son aliyemalizia kazi kwa kuandika bao la tatu dakika mbili baada ya kuanza kipindi cha pili na hivyo kuihakikishia Tottenham ushindi mnono dhidi ya mahasimu wao wa London.
Wakati, Arteta akitoa malalamiko hayo, kocha wa Tottenham, Antonio Conte amesema kwamba kocha mwenzake huyo analalamika sana.
“Nataka waamuzi wajitokeze mbele ya kamera na kuelezea uamuzi wao, ni aibu kwani mchezo mzuri umeangamizwa leo (jana), hatufurahii hili mimi na wachezaji wangu, najivunia wachezaji wangu, uamuzi umeshafanyika hatuwezi kuubadili, waamuzi wanatakiwa kufanya uamuzi katika soka,” alisema Arteta.
“Kwa sasa tunaifikiria mechi yetu na Newcastle, mechi hii ni historia, imepita, imetoka mikononi mwetu na tunatakiwa kukubali, sasa tunatakiwa kuwa timu ambayo mliiona kuanzia mwanzo.”
“Unapopoteza mechi katika mazingira haya inauma sana, lakini tuna mechi kubwa Jumatatu kwa hiyo tutajitahidi kushinda, tuna mechi mbili mikononi mwetu na sasa tunataka kufanya kazi yetu.”
Akizungumzia hoja za Arteta, Conte alisema, “Arteta ni kocha mzuri, anaweza kuwa kocha muhimu siku zijazo lakini katika kipindi cha miezi sita nimekuwa nikimsikiliza akilalamika mno.
“Ndio kwanza ameanza kazi yake na nimekuwa nikimsikiliza akilalamika sana, nafikiri anatakiwa kuwa makini na kazi yake kwenye timu yake na si kulalamika, nafikiri anatakiwa kutulia na kujaribu kuendelea na kazi yake kwa sababu yuko vizuri lakini kocha kulalamika sana si jambo zuri.”
Matokeo ya jana yanakuwa pigo kwa Arteta hasa inapozingatiwa kauli aliyoitoa kabla ya mechi hiyo kwamba nafasi yao ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao ilikuwa kwenye ushindi dhidi ya Tottenham.
Kimataifa Arteta: Waamuzi wanaharibu soka
Arteta: Waamuzi wanaharibu soka
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
