Lima, Peru
Kocha wa timu ya taifa ya Argentina, Lionel Scaloni amewashangaa wanaohoji kustaafu kwa Lionel Messi kwenye timu ya taifa akidai kwamba yeye hawezi kupanga siku ya mchezaji huyo kustaafu.
Messi, 36, mwishoni mwa mwaka jana aliiongoza Argentina kubeba Kombe la Dunia, amekuwa akihusishwa na mpango wa kustaafu soka la kimataifa lakini mwenyewe hajasema lini atachukua uamuzi huo.
Alipoulizwa katika mkutano na waandishi wa habari, jana Jumatatu kuhusu mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Peru kama atajizoeza kupanga timu bila ya Messi, kocha huyo alisema, “Tuweke katika akili zetu kwamba Messi bado yuko na timu hii.”
“Ya nini kufikiria kuhusu siku ya kuondoka kwake, ukweli ni kwamba bado ana nguvu, tumuache, je tumeamua kuanza kumstaafisha, tunaharakisha mambo, ajabu,” alisema Scalloni.
Alhamisi iliyopita, Messi ambaye ni nahodha wa Argentina alianzia benchi na kuingia dakika ya 40 katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Paraguay, mechi ambayo Argentina ilishinda kwa bao 1-0.
Mwezi uliopita, Messi aliichezea Argentina na kufunga bao katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Ecuador lakini akakosekana katika mechi iliyofuata dhidi ya Bolivia ambayo Argentina ilishinda kwa mabao 3-0.
Katika siku za karibuni, Messi amekuwa akisumbuliwa na tatizo la misuli na licha ya matatizo hayo, Scalloni aliweka wazi nafasi ya mchezaji huyo katika timu yake ambayo kesho Jumatano itaumana na Peru.
“Messi yuko vizuri, amekuwa akiongeza dakika za mazoezi, tutafanya uamuzi Jumanne, ni suala la dakika anazoongeza na atacheza kwa muda gani, kama yuko vizuri mnajua ninachokifikiria, atacheza,” alisema Scaloni.
