Barcelona, Hispania
Mshambuliaji wa Barcelona, Robert Lewandowski ataikosa mechi dhidi ya mahasimu wao Real Madrid maarufu El-Clasico itakayopigwa keshokutwa Alhamisi baada ya kuumia mguu katika mechi na Almeira.
Lewandowski, mshambuliaji tegemeo wa Barca kukosekana kwake katika mechi hiyo kunaiongezea majanga timu yake ambayo katika mechi hiyo ya La Liga dhidi ya Almeira ililala kwa bao 1-0.
Matokeo hayo ya kushtusha yameifanya Barca inayoshika usukani katika La Liga kushindwa kuongeza tofauti ya pointi kufikia 10 dhidi ya Real Madrid inayoshika nafasi ya pili.
Mechi hiyo ya wababe wa Hispania itakayopigwa Alhamisi ni ya nusu fainali ya kwanza ya Kombe la Mfalme maarufu Copa del Rey na huenda Lewandowski tena akaikosa mechi ya La Liga dhidi ya Valencia wikiendi ijayo.
Baada ya hapo, Barca itaumana kwa mara nyingine na Real Madrid katika mechi ya La Liga ambayo itapigwa Machi 19 kwenye dimba la Nou Camp, mechi ambayo huenda Lewandowski akawa fiti kwa ajili ya kucheza.
Taarifa ya Barca kuhusu Lewandowski ilieleza kwa kifupi, “Robert Lewandowski amepata matatizo ya misuli ya mguu wa kushoto, mchezaji huyo kutoka Poland hatokuwa uwanjani hadi tatizo litakapoisha.”
Awali Lewandowski alipewa adhabu na kukosa mechi tatu za mwezi Januari na Barca ikawa katika wakati mgumu kwa kumkosa mtu sahihi wa kuziba pengo lake baada ya kuwaruhusu Pierre-Emerick Aubameyang na Memphis Depay waihame klabu hiyo.
Timu hiyo pia inawakosa Pedri na Ousmane Dembele ambao ni majeruhi, Dembele alicheza mara ya mwisho Januari mwishoni dhidi ya Girona wakati Pedri amekuwa nje tangu aumie Februari 16 katika mechi dhidi ya Man United.
Barca pia itamkosa Gavi katika mechi na Valencia kwa kuwa mchezaji huyo atakuwa akitumikia adhabu ya kukosa mechi moja kama ilivyo kwa kocha Xavi.
Kimataifa Lewandowski kuikosa El Clasico
Lewandowski kuikosa El Clasico
Read also