Na mwandishi wetu
Klabu ya soka ya Simba imetangaza kuachanana winga wake Ladack Chasambi ambaye sasa ni rasmi hatokuwa na timu hiyo kwa msimu ujao wa 2026-27.
Taarifa iliyopatikana Jumamosi Julai 18, 2026 kwenye vyanzo vya habari vya klabu hiyo, imemtaja mchezaji huyo kuwa mmoja wa wachezaji ambao wamepewa nafasi ya kutafuta maisha nje ya Simba.
Chasambi alijiunga na Simba Januari 2024 akitokea Mtibwa Sugar ambapo alipandishwa katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo baada ya kuonesha uwezo wake kwenye timu ya vijana kabla ya Simba kuvutiwa naye.
Alisajiliwa na Simba wakati huo ikiwa chini ya kocha Abdelhak Benchikha akitajwa kuwa mmoja wa wachezaji waliopewa matumaini makubwa ya kutamba kutokana na uwezo alioanza kuuonesha.
Hali hata hivyo imekuwa tofauti kwa mchezaji huyo ambaye hatimaye Simba imetangaza rasmi kuachana naye.
Chasambi sasa anaungana na mshambuliaji wa timu hiyo, Jonathan Sowah ambaye naye alitangaza kuachwa baada ya kuichezea timu hiyo kwa msimu mmoja tu akitokea Singida Black Stars.
Mchezaji mwingine ambaye Simba imetangaza kuachana naye hivi karibuni ni kiungo mkongwe, Muzamir Yassin ambaye amekuwa na timu hiyo akicheza kwa mafanikio kwa takriban miaka 10.
Soka Chasambi aachwa Simba
Chasambi aachwa Simba
Read also
