Na mwandishi wetu
Mabao ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Bakari Mwamnyeto yameiwezesha Yanga kunyakua pointi tatu muhimu dhidi ya Ruvu Shooting katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa Jumatatu usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kwa ushindi huo, Yanga sasa wanafikisha pointi 13 sawa na mahasimu wao Simba ambao wanapambana kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo Simba wakiwatangulia kwa tofauti ya mabao ya kufunga wakati Ruvu wanabaki na pointi zao tano.
Feisal Salum au Fei Toto ambaye amezoeleka kwa kufunga mabao ya mashuti ya mbali ndiye aliyeipatia Yanga bao la kwanza dakika saba baada ya kuanza kipindi cha pili akiunganisha kwa kichwa mpira uliopigwa na Joyce Lomalisa.
Mwamnyeto aliiandikia Yanga bao la pili katika dakika ya 71 akiunganisha kwa kichwa kona ya Dickson Ambundo ambaye aliingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Farid Mussa.
Bao pekee la Ruvu Shooting lilipatikana zikiwa zimebaki dakika tano kabla ya mpira kumalizika mfungaji akiwa ni Roland Msonjo akiujaza wavuni mpira ambao kwanza uliokolewa kwa kichwa na Lomalisa kabla ya kumkuta mfungaji.
Katika mechi hiyo Ruvu Shooting walicheza mechi hiyo kwa tahadhari kubwa wakijihami na wakati mwingine kutengeneza mashambulizi ya kushtukiza pale walipopata nafasi ya kufanya hivyo.
Nayo Coastal Union ikiwa nyumbani katika mechi nyingine ya Ligi Kuu NBC iliibugiza Kagera Sugar mabao 2-0, mabao ya washindi yakifungwa na Moubarack Hamza katika dakika za tisa na 64, ushindi ambao unaifanya Costal kufikisha pointi saba katika mechi sita.
Katika mechi nyingine bao pekee la Sospter Bajana liliiwezesha Azam kutoka uwanjani na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Singida Big, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Chamazi, matokeo ambayo yanaifanya Azam kufikisha pointi nane.
Ligi hiyo itaendelea leo kwa mechi ziafuatazo…
Polisi v Geita Gold
Ihefu v Prisons
Soka Fei Toto, Mwamnyeto waibeba Yanga
Fei Toto, Mwamnyeto waibeba Yanga
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
