Na mwandishi wetu
Baada ya jana Yanga kumalizana na Biashara United kwenye mchezo ulioisha kwa sare ya bao 1-1, timu hiyo leo mapema imekwenda mkoani Shinyanga kujichimbia ikijipanga kwa ajili ya mchezo wao wa nusu fainali ya Kombe la Azam (ASFC).
Yanga imekwenda mkoani humo kujiandaa na mechi hiyo itakayopigwa Jumamosi hii dhidi ya mahasimu wao, Simba kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze amesema baadhi ya mambo watakayokwenda kujipanga nayo ni makosa waliyoyabaini kwenye mechi zao mbili za ligi zilizopita na kuyafanyia kazi ili yasijirudie watakapoumana na Mnyama.
“Nadhani mechi za kama hivi za ‘derby’ hauna haja ya kuwapa hamasa nyingi wachezaji kwa sababu tayari ni jambo kubwa na zaidi ni kukaa na kuangalia makosa yetu, naamini mechi ya Biashara na iliyopita (dhidi ya Mbeya Kwanza walioshinda 4-0) tumeruhusu sana mpinzani kujiamini na mpira na kufika eneo letu.
“Sasa ukifanya makosa kama hayo kwa wachezaji wenye uzoefu na mbinu nzuri unaweza ukapata matatizo, hivyo cha kwanza tutakaa kufanya uchambuzi wa kwetu kuona tunafanyaje kuelekea mchezo wa Jumamosi,” alisema Kaze.
Wakati Yanga ikiingia Shinyanga, Simba nayo imeripotiwa kwenda Wilaya ya Misungwi, Mwanza kuendelea na kujipanga kwa ajili ya mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu ya kumtafuta nani mbabe baada ya sare mbili za mechi za ligi walizokutana msimu huu.
Simba ndiyo bingwa mtetezi wa kombe hilo baada ya msimu uliopita kuifunga Yanga bao 1-0 kwenye fainali iliyopigwa Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Wakati huo huo, TFF imetangaza viingilio vya mechi hiyo ambavyo ni kuanzia Sh 30,000 kwa VIP A, Sh 20,000 kwa VIP B na Sh 10,000 kwa mzunguko.
Soka Yanga yajichimbia Shinyanga ikiisubiri Simba
Yanga yajichimbia Shinyanga ikiisubiri Simba
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
