Na mwandishi wetu
Klabu ya soka ya Coastal Union inazidi kujiimarisha kwa ajili ya msimu ujao wa 2022/23 baada ya leo kumtambulisha kiungo mshambuliaji Riguene Pembele raia wa DR Congo.
Mchezaji huyo anayeelezwa kusajiliwa kutoka Don Bosco ya nchini kwao amemwaga wino wa kuwatumikia Wagosi wa Kaya hao kwa mkataba wa miaka miwili baada ya uongozi wa timu hiyo kuridhishwa na kiwango chake.
Ofisa Habari wa Coastal, Jonathan Tito ameeleza kuwa safari hii usajili wao umelenga zaidi wachezaji wanaokipiga timu za taifa kama ilivyo kwa Pembele kwa kuwa wanaunda kikosi chenye ushindani maradufu kuelekea msimu ujao.
“Ujio wa Pembele kwetu una maana kubwa kutokana na kiwango chake na tumekuwa tukimfuatilia kwa muda sasa kabla ya kujiridhisha kumsajili, baadhi ya watu wetu ambao wanaufahamu mpira waliupa uongozi taarifa juu yake na baada ya kujiridhisha tumemchukua.
“Kiuhalisia bado hatujamaliza usajili, tutaendelea na zoezi hilo kwa sababu tuna wachezaji sita tutawatambulisha na wote ni wachezaji wenye tija, baada ya hapo tutakuwa tumefunga usajili tayari sasa kwa msimu ujao,” alisema Tito.
Mbali na Pembele anayemudu kucheza winga ya kushoto, kulia na kiungo mshambuliaji wa kati, wengine waliotambulishwa na timu hiyo ni Khatib Kombo kutoka Kipanga FC ya Zanzibar, kiungo mshambuliaji wa KMKM, Optatusy Lupekenya na mshambuliaji Omar Mbaruk kutoka Fountain Gate.
Pia yumo kiungo mshambuliaji, Djibril Olatoundji kutoka ASVO Benin, mshambuliaji kutoka KVZ ya Zanzibar, Maabad Maulid pamoja na kipa wa timu ya taifa ya Comoro, Mahmoud Mroivili.
Soka Pembele wa DR Congo asaini Coastal
Pembele wa DR Congo asaini Coastal
Read also