Na mwandishi wetu
Uongozi wa timu ya Kagera Sugar umeeleza uzoefu na ubora wa kazi ya Fred Felix Minziro ndivyo vilivyopelekea wakampa ukocha mkuu wa timu hiyo kwa muda wa mwaka mmoja.
Akizungumza na GreenSports, Katibu Mkuu wa Kagera Sugar, Ally Masoud alisema wamemchukua Minziro wakiamini kile alichonacho na rekodi alizonazo katika kuzifundisha timu mbalimbali za Ligi Kuu NBC.
“Minziro ni kocha mwenye rekodi nyingi na uzoefu wa kutosha katika kufundisha timu za Ligi Kuu Tanzania Bara, hicho ndio kimetuvutia na kuamua kumkabidhi kikosi chetu tukiamini atatufikisha tulipokusudia,” alisema Masoud.
Kiongozi huyo alisema kwa kutumia uwezo wake yeye na wenzake wanaamini ataitoa timu yao kwenye nafasi mbaya na kuwaweka nafasi za juu na salama kwao.
Naye Minziro alisema: “Nawashukuru viongozi wa Kagera Sugar kwa kuniona nafaa kuifundisha timu yao, naahidi kuitumia vizuri nafasi hii kwa kuirudisha kwenye mbio za ubingwa lakini ili tufanikiwe hayo naomba ushirikiano kuanzia viongozi hadi wachezaji,” alisema Minziro.
Minziro kabla ya kutambulishwa Kagera jana Jumatano, alikuwa akiinoa Tanzania Prisons ambayo ilimfuta kazi mwezi mmoja uliopita kutokana na matokeo mabaya iliyokuwa ikiyapata timu hiyo.