Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imedai kukamilisha maandalizi ya mchezo wake dhidi ya Al Hilal kwa asilimia 90 huku ikiwasihi mashabiki wake kujitokeza kwa wingi Jumamosi kuwaunga mkono.
Yanga itacheza mechi ya mkondo wa kwanza hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam dhidi ya Al Hilal kutoka Sudan, Jumamosi hii.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe alisema kuwa kikosi hicho kimekamilisha maandalizi yao, hakuna majeruhi na hata waliokuwa nje ya kikosi kama nyota wao Stephane Aziz Ki naye ameshajiunga kwenye mazoezi ya kikosi hicho yanayoendelea Avic Town, Kigamboni.
Kuhusu Aziz ambaye alikuwa kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Burkina Faso, imeelezwa kuwa amechelewa kujiunga na kikosi hicho hata baada ya majukumu hayo akidaiwa kukumbwa na Covid-19 lakini sasa yuko vizuri.
“Zaidi ya asilimia 90 ya maandalizi ya mechi yetu na Al Hilal yanakwenda vizuri, kwenye maandalizi yote mengine hata ya kuwapokea wageni wetu (Hilal) yameshafanywa pia.
“Hali ya kambi mpaka sasa hakuna aliyepata majeraha, waliochelewa kuripoti kambini kama Aziz Ki tayari amewasili na amejiunga moja kwa moja na maezozi, hivyo kocha Nabi (Nasreddine) hana mengi zaidi ya kuwaomba wanachama na mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu siku ya mechi,” alisema Kamwe.
Naye Rais wa Yanga, Hersi Said ameeleza namna gani mchezo huo ulivyo mgumu na muhimu kwao ambao utawapa matokeo na taswira mpya juu ya kikosi hicho kwenye michuano hiyo ambayo wamepania kutinga hatua ya makundi baada ya kutofanya hivyo kwa miaka 24 sasa.
“Mechi hiyo tunatarajia itakuwa muhimu sana na ngumu pia kwa sababu Hilal ni moja ya timu kubwa zenye historia nzuri lakini ni miongoni mwa timu ambazo naamini itakuwa ni kipimo tosha kwa Wanayanga sasa kuiona timu yao imefikia ukubwa kiasi gani.
“Nichukue nafasi hii kuwaalika mashabiki na wanachama, mechi hii ni muhimu kwa timu yetu na kama kweli tunahitaji ushindi, ningependa Yanga tuujaze Uwanja wa Mkapa, ningependa wachukue nguvu kubwa waliyonayo kama mchezaji wa 12 kuhakikisha wanaujaza uwanja na kuwapa sapoti wachezaji wetu ya kuibuka na ushindi,” alisema Said.
Soka Hersi awaita mashabiki Yanga Kwa Mkapa
Hersi awaita mashabiki Yanga Kwa Mkapa
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
