Na mwandishi wetu
Licha ya kufungwa mabao 3-2 na Geita Gold, timu ya Ruvu Shooting imeeleza kuwa bado ina nafasi ya kuendelea kupambana kuhakikisha inatoka kwenye mstari wa kushuka daraja.
Kocha wa Ruvu, Mbwana Makata ameeleza kuwa ingawa walipambana na kuchomoa mabao mawili waliyotanguliwa lakini makosa ya dakika za mwisho yaliwaponza na kuwapa bao wapinzani wao licha ya kuwa vijana wake walijituma mno.
Alisema kwa matokeo hayo bado wana nafasi, wanakwenda kujipanga zaidi kwa mchezo unaofuata dhidi ya Kagera Sugar wakitaka kurekebisha makosa, wapate matokeo na kujitoa mkiani mwa msimamo wa ligi.
“Mechi hiyo imeshapita na sasa akili zetu zimehamia kwenye mechi na Kagera na zinazofuata, tunarekebisha makosa ili kufufua matumaini ya kuepuka kushuka daraja, nina imani tukishinda mechi mbili tatu tutasogea juu na tutapambana mpaka mwisho tuone kilichopo, kwa sasa bado mapema sana,” alisema Makata.
Naye kocha msaidizi wa Geita Gold, Mathias Wandiba alisema wanawashukuru wachezaji kwa kujituma kwao na kupata matokeo kwa kuwa mchezo ulikuwa mgumu kutokana na mazingira halisi ya Ruvu kuhitaji pointi ili kujinasua mkiani, pia aliwashukuru mashabiki wao kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono uwanjani.
Ruvu ipo nafasi ya 15 ikiwa na pointi 17 wakati Geita ipo nafasi ya tano na ina pointi 34 baada ya wote kushuka dimbani mara 23.