Rabat, Morocco
Kocha wa zamani wa Yanga ya Tanzania ambaye kwa sasa anainoa timu ya taifa ya Mali, Tom Saintfiet amelijia juu Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa uamuzi wa kuzifanya fainali za Afcon zichezwe kila baada ya miaka minne.
Saintfiet, kocha mzaliwa wa Ubelgiji aliyeinoa Yanga mwaka 2012, ameutaja uamuzi huo kuwa umetokana na Umoja wa Vyama vya Soka Ulaya (Uefa) pamoja na Fifa na hautokani na mapenzi ya moyoni ya soka barani Afrika.
Uamuzi wa kuifanya Afcon kuwa michuano ya miaka minne badala ya miwili iliyozoeleka ulitangazwa Jumamosi na Rais wa CAF, Patrice Motsepe katika mkutano na waandishi wa habari.
Motsepe katika mkutano huo pia alitangaza uzinduzi wa michuano mipya ya African Nations League (Ligi ya Mataifa ya Afrika) ambayo itakuwa ikifanyika kila mwaka.
Saintfiet, 68, ambaye timu yake kesho Ijumaa itaumana na wenyeji Morocco katika fainali zinazoendelea za Afcon 2025, alieleza kushtushwa kwake na uamuzi huo ambao alisema anaamini umelikosea heshima soka la Afrika.
“Nimeshtushwa na uamuzi huu, umenikatisha tamaa ni uamuzi ambao umetokana na maelekezo ya mabosi wa Uefa, klabu kubwa kutoka ligi tano duniani, pamoja na Fifa, na hilo linanisikitisha,” alisema Saintfiet.
Saintfiet alisema wamepambana sana kutaka heshima ya Afrika kwa watu wa Afrika na Afrika iwe na utambulisho wake na kuheshimika lakini Afrika wanaishia kusikiliza mambo ya Ulaya na kubadili historia kwa sababu ya fedha na kuamua kucheza Afcon kila baada ya miaka minne.
Kocha huyo ambaye pia amewahi kufundisha soka nchi kadhaa zikiwamo Jordan, Ujerumani, Finland, Qatar na nyinginezo barani Afrika, alisem licha ya kusikitishwa na uamuzi huo, anaamini mapenzi ya soka la Afrika yatashinda presha za kutoka Ulaya.
Kwa upande wa Motsepe alisema sababu mojawapo ya mabadiliko katika michuano hiyo pamoja na mambo mengine ni kupunguza migogoro ya mara kwa mara kati ya klabu na timu za taifa wakati zinapokaribia fainali za Afcon.
Motsepe pia alisema shauku ya kuongeza mapato pia imechangia mabadiliko hayo ya Afcon kuchezwa kila baada ya miaka minne badala ya miwili, uamuzi ambao unatarajia kuanza baada ya fainali za mwaka 2028.
