Cairo, Misri
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limetaka Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya mmiliki na mwenyekiti wa klabu ya Napoli ya Italia, Aurelio De Laurentiis ambaye amesema timu yake haitosajili wachezaji wa Afrika kwa sababu ya ushiriki wao kwenye Afcon.
De Laurentiis hivi karibuni alinukuliwa na vyombo vya habari akitoa kauli iliyoonekana kuwa na utata aliposema kwamba klabu yake haitosajili wachezaji kutoka Afrika hadi wachezaji hao watakapokubali kujitoa kushiriki kwenye fainali za Afcon, michuano ya soka inayoshirikisha mataifa ya Afrika.
“CAF imeshitushwa na kauli iliyokosa umakini na isiyokubalika ambayo imetolewa na kiongozi wa klabu ya Napoli, Aurelio De Laurentiis kuhusu wachezaji wa Afrika na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon),” ilieleza taarifa ya CAF.
“Kwa kutangaza hadharani kwamba wachezaji watakaosajliwa na Napoli ni lazima watangaze kujitoa ushiriki wao kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kama kigezo cha kuajiriwa, kauli hiyo ya De Laurentiis inaangukia katika Ibara ya 14 ya kanuni za kinidhamu za Uefa, kwa hiyo tunaishauri Uefa kuanza uchunguzi wa kinidhamu dhidi ya kiongozi huyo,” ilifafanua taarifa ya CAF.
CAF inaamini kuwa kauli za De Laurentiis ni za kibaguzi na zinaibua maswali iwapo bosi huyo wa Napoli anaweza kuchukua hatua hizo hizo kwa wachezaji wa mabara mengine.
“Je tujenge fikra kwamba kiongozi wa Napoli ataweka vigezo hivyo hivyo kwa wachezaji wa Marekani ya Kusini, Asia na wa mashirikisho mengine kuwazuia kushiriki mashindano ya kwenye mashirikisho yao, mashindano ambayo ni muhimu kwa maendeleo na ukuaji wa soka duniani kote,” alieleza taarifa ya CAF na kuzitaja fainali za Afcon kuwa ni mashindano muhimu na makubwa kwa miaka mingi sasa.
“Mashindano ya Mataifa ya Afrika yanalibeba bara la Afrika na ni moja ya mashindano ya soka yanayoongoza duniani, mara ya mwisho mashindano yalifanyika Cameroon na kuonyeshwa katika nchi zaidi ya 160 na kushuhudiwa kwenye televisheni na watu zaidi ya milioni 600.” ilieleza taarifa ya CAF.
Fainali za Afcon hufanyika mara moja kila baada ya miaka miwili, kutokana na janga la Corona, mashindano ya 2021 yalifanyika mapema mwaka huu na Senegal kuibuka vinara na fainali za mwakani zilizopangwa kufanyika Juni 2023 nchini Ivory Coast, zimehamishiwa Januari 2024 ili kukwepa msimu wa mvua katika nchi hiyo.
Kimataifa CAF yataka bosi Napoli aadhibiwe
CAF yataka bosi Napoli aadhibiwe
Read also