Madrid, Hispania
Angeles Bejar ambaye ni mama wa rais wa Shirikisho la Soka Hispania (REEF) aliyesimamishwa, Luis Rubiales amekimbizwa hospitali akiwa hoi baada ya kuwa katika mgomo wa kula akishinikiza mwanaye asibughudhiwe.
Mama huyo alichukua uamuzi wa kugoma kula tangu Jumatatu na kujihifadhi kanisani akifanya maombi kwa alichodai kuwa mwanaye amekuwa akisakamwa kwa madai ya kumbusu mdomoni mshambuliaji wa timu ya Hispania, Jenni Hermoso.
Rubiales amejikuta akishutumiwa na kushinikizwa ajiuzulu kwa kumbusu mdomoni Jenni wakati wa shamrashamra za timu ya Hispania kubeba Kombe la Dunia baada ya timu hiyo kuichapa England bao 1-0 katika mechi ya fainali.
Katika tukio hilo lililotokea Agosti 20, awali Jenni (pichani chini) alidaiwa kumtetea Rubiales lakini baadaye alisema kwamba hakupenda alichofanyiwa na kiongozi huyo kwani hakuwa ameridhia kufanyiwa hivyo.
Akiwa kanisani mama Angeles aliahidi kuendelea na mgomo wa kula usiku na mchana bila ukomo lakini jana Jumatano hali yake ilikuwa mbaya na kulazimika kuwahishwa hospitali na hivyo kusimamisha mgomo wa kula kwa muda.
“Unyama na mashambulizi ambayo anafanyiwa mwanangu ni jambo ambalo hapaswi kukutana nalo,” alisema mama huyo.
“Amepelekwa hospitali na kulazimika kusimamisha mgomo wa kula, amekuwa si mwenye kujisikia vizuri kutokana na joto na matatizo mengineyo, miguu yake imelegea na amekuwa katika uchovu,” alisema mchungaji mmoja wa kanisa hilo aliyetajwa kwa jina moja la Antonio.
Jumamosi iliyopita, Rubiales alisimamishwa kwa siku 90 na Fifa wakati uchunguzi wa kadhia inayomkabili ukiendelea wakati baadhi ya viongozi wa soka Hispania wakimshinikiza ajiuzulu.
Wachezaji 81 wa timu ya wanawake wa Hispania wametangaza kutokuwa tayari kuichezea timu hiyo kama Rubiales ataendelea kuwa kiongozi wa REEF.
Rubiales awali alijitetea akisema kwamba alichokifanya kilitokana na furaha isiyo kifani na kutaka wenye mtazamo tofauti na tukio hilo wapuuzwe ingawa baadaye aliomba radhi lakini amekataa kujiuzulu akidai kwamba hakumbusu Jenni kwa kumlazimisha.