Paris, Ufaransa
Wakati habari ya Messi kurudi Barca ikijadiliwa, kocha wa zamani wa timu hiyo, Pep Guardiola amesema mchezaji huyo akirudi katika klabu hiyo atakuwa amefanya jambo kubwa la aina yake.
Pep ambaye kwa sasa anainoa Man City, akiwa kocha wa Barca, Messi alikuwa mmoja wa wachezaji wake muhimu walioiwezesha timu hiyo kuweka rekodi ya mataji matatu ya La Liga na mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Messi ataihama klabu yake ya sasa ya PSG ya Ufaransa mara baada ya mkataba wake kumalizika msimu huu lakini wapi anakwenda ni mjadala unaoendelea kuteka hisia za mashabiki wa soka duniani.
Baba mzazi wa mchezaji huyo Jorge, Messi hivi karibuni alikanusha habari kwamba mchezaji huyo ana makubaliano ya kujiunga na klabu ya Al Hilala ya Riyadh, Saudi Arabia msimu ujao.
Vyanzo mbalimbali vya habari vimekuwa vikidai kuwa Messi, ambaye ni balozi wa utalii wa Saudi Arabia ana makubaliano maalum na Al Hilal ambao ni mahasimu wa klabu nyingine ya Riyadh ya Al Nassr anayoichezea Cristiano Ronaldo.
“Mimi ni shabiki wa Barcelona, nina tiketi za msimu (Nou Camp) na nina matumaini kwamba kuna siku tutamuaga rasmi kwani ana haki ya kufanyiwa hivyo, ni mchezaji bora wa wakati wote,” alisema Pep.
“Katika miaka 12 au zaidi Barcelona ilikuwa juu, na hilo lisingewezekana bila ya yeye (Messi) na hapa sizungumzii namba badala yake ni uhusika wake katika uchezaji, ubora wake, umakini na kila kitu,” alisema Pep.
Messi ambaye hivi karibuni alipewa adhabu ya kufungiwa wiki mbili, PSG imemfutia adhabu hiyo baada ya kuomba radhi na anatarajia kuichezea timu hiyo kesho Jumamosi katika mechi ya Ligi I dhidi ya Ajaccio.