Na mwandishi wetu
Makocha wa Simba na Yanga kila mmoja amejinadi kuonesha soka safi na la ushindani hapo kesho katika mechi hiyo maarufu Dar au Kariakoo Derby kwa ajili ya kuwapa raha mashabiki wa timu hizo.
Mtanange huo wa kwanza msimu huu kwa timu hizo katika Ligi Kuu ya NBC utapigwa majira ya saa 11 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi akizungumza leo alisema anafahamu ukubwa wa mechi hiyo na kwamba wamejiandaa kisawasawa kwa utulivu mkubwa, kwa kujituma huku wakimheshimu mpinzani wanayekutana naye.
Pamoja na hayo, Nabi pia alitumia nafasi hiyo kuwaomba radhi mashabiki wa Yanga kwa matokeo ya kushindwa kuingia hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika wakitolewa na Al Hilal ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-1.
“Tumejiandaa kutokana na mechi ya kesho, tumesahau yote yaliyopita, kimpira huzungumzii yaliyopita labda umemfunga Simba mara ngapi au umetoa sare ngapi, refa akipiga filimbi ya kumaliza mpira na yale yamekwisha na yale ya kutolewa na kufuzu ni kitu kimoja tu sababu yote ni soka.
“Lakini kwa upande wangu na benchi tunaomba msamaha mashabiki sababu haikuwa malengo kutolewa ila imetokea bahati mbaya tumejitahidi lakini haikuwa hivyo, tutajitahidi kadri ya uwezo wetu kuwafurahisha mashabiki wa Yanga na kuwarudishia furaha yao,” alisema Nabi.
Pia, Nabi aliwataka wapenda soka wajiandae kushuhudia soka safi la kutembeza pasi kwa kuwa ndiyo mtindo wake huku akiwashukuru asilimia kubwa ya mashabiki wa Yanga waliokuwa wakimtia moyo hivi karibuni alipokuwa akipitia kipindi kigumu, hivyo hayo yote yanampa sababu ya kuwafurahisha Wanayanga hiyo kesho.

Naye kocha wa Simba, Juma Mgunda amesema kuwa kesho watacheza soka la ushindani kwa kuwa mazingira ya mechi yanawaruhusu kufanya hivyo kutokana na ushindani uliopo baina yao, akisisitiza kuwa wamejiandaa vya kutosha kuonesha soka la pasi na kutembeza mpira.
“Kwa ujumla tutacheza mechi ya ushindani sababu Yanga na Simba hakuna asiyejua ni wapinzani, kwa hiyo si mechi rahisi tunalitambua hilo, tunafahamu hivyo kwa hiyo maandalizi yote ya kucheza na timu nzuri, yenye walimu wazuri, wachezaji wazuri wenye ushindani tumeyachukua kwa ajili ya mechi muhimu kama ya kesho.
“Ni kweli nimechukua timu wakati kuna mechi mbili au tatu Simba haikufanya vizuri kwa Yanga, najua Wanasimba wanataka nini, najua vijana wangu wanataka nini, tumejiandaa vizuri kupambana na wenzetu naamini mechi za derby zina utaratibu wake na ushindani wake na pamoja na ushindani mkubwa lakini mpira utatembea kesho,” alisema Mgunda.
Timu hizo kesho zitaingia uwanjani zikiwa timu mbili pekee ambazo hazijapoteza mchezo tangu kuanza msimu huu baada ya kucheza mechi tano, zikishinda nne na kutoa sare mechi moja kila mmoja.
Simba inaongoza ligi ikifuatiwa na Yanga wote wakiwa na pointi 13 isipokuwa Wekundu hao wamezidiwa na Yanga kwa mabao ya kufungwa. Yanga imefungwa mabao manne, Simba imefungwa mawili huku wote wakitikisa nyavu mara 11.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii wa kufungua pazia la ligi msimu huu na Simba ikapoteza kwa mabao 2-1.
Kabla ya hapo, msimu uliopita timu hizo za Kariakoo zilikutana mara nne ambapo kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, Yanga ilishinda bao 1-0, kwenye mechi mbili za ligi ziliisha kwa suluhu kabla ya kukutana tena kwenye nusu fainali ya Kombe la FA na Yanga ilitoka kifua mbele kwa bao 1-0.
