Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Pyramids FC, Fiston Mayele ametinga katika hoteli waliyofikia Simba nchini Misri kwa ajili ya mechi yao ya mkondo wa pili ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly.
Mayele aliyewahi kukipiga Yanga, aliwatembelea mahasimu wake hao wa zamani na kuonana na baadhi ya wachezaji na viongozi wa timu hiyo ambao alisalimiana nao na kubadilishana nao mawazo.
Katika video iliyowekwa leo Alhamisi na mtandao wa Simba, Mayele raia wa DR Congo alionekana akisalimiana na wachezaji wa Simba akiwemo Fabrice Ngoma ambaye alionekana akimtania kuwa anapaswa kujiunga na Wekundu hao.
Mfungaji huyo bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita alionekana mwenye furaha kuonana na ‘nduguze’ hao aliokuwa akishindana nao kwenye Ligi Kuu NBC huku akiwatakia kila la heri katika mechi yao hiyo itakayopigwa kesho Ijumaa, Uwanja wa Cairo, mjini Cairo.
Katika mchezo huo, Simba inahitaji ushindi ili kusonga hatua ya nusu fainali baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kwenye mechi ya awali iliyopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam wiki iliyopita.
Kimataifa Mayele awatembelea Simba Misri
Mayele awatembelea Simba Misri
Read also
