Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ (pichani) amewataka wachezaji wake kutobweteka na hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kwani kazi iliyopo mbele yao ni ngumu zaidi.
Simba ni miongoni mwa timu nane Afrika zilizofika robo fainali baada ya kufanya vizuri kwenye mechi za hatua ya makundi ikiwemo kutoa kipigo cha mabao 7-0, dhidi ya Horoya AC ya Guinea.
Kocha huyo raia wa Brazil ameeleza kuwa ugumu wa hatua wanayoielekea unatokana na ubora na uzoefu wa timu zilizofuzu hatua hiyo, hivyo inahitaji utulivu na umakini wa hali ya juu ili kupata kile walichokikusudia.
“Nawapongeza wachezaji wangu kwa jitihada walizozifanya hadi tulipofika, lakini wanapaswa kusahau yaliyopita sababu tumeingia hatua nyingine ambayo inahitaji umakini wa hali ya juu ili kufikia malengo yetu,” alisema Robertinho.
Alisema anajua uzito wa hatua waliyopo lakini kama wachezaji wake watacheza kwa kujituma na hakuna kitu ambacho kitashindikana na hilo alilisema siku ya kwanza wakati akitambulishwa.
“Sitaki kujua ukubwa au mafanikio ya timu tutakayopangiwa kwenye hatua inayofuata ninachokifanya ni kuiandaa timu yangu kwa ajili ya kukabiliana na chochote na hilo linawezekana kama wachezaji watajitoa na kufanyia kazi maelekezo ninayowapa kwenye uwanja wa mazoezi,” alisema Robertinho.
Kocha huyo ameeleza kuwa uwezekano wa Simba kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu upo endapo tu umoja na ushirikiano uliopo ndani ya timu hiyo utaongezeka zaidi ya ilivyokuwa kwenye hatua ya makundi.