Na mwandishi wetu
Nahodha wa Simba Queens, Opa Clement amesema tuzo mbili za mchezaji bora wa mwezi alizobeba mfululizo zimempa hamasa ya kuendelea kupambana zaidi kuipigania timu na kutimiza ndoto zake.
Opa ametwaa tuzo za mchezaji bora wa mwezi Desemba na Januari msimu huu ambapo licha ya kuandika rekodi hiyo pia ametwaa Sh 100,000 na taulo za kike za Rani kama zawadi kwa tuzo hiyo.
Mshambuliaji huyo alisema ana furaha mno kufanikiwa kuchukua mara mbili tuzo hiyo na zaidi akiwashukuru wachezaji wenzake ambao ushirikiano wao kwake ndiyo umepelekea mafanikio hayo.
“Namshukuru Mungu kwanza na pia nina furaha sana kuchukua tuzo ya Desemba na Januari, nawashukuru wachezaji wenzangu sababu bila wao nisingekuwa bora, ndiyo wamenifanya niwe bora, pia inanipa motisha ya kuongeza juhudi ya kupambana, kuipambania timu yangu,” alisema Opa.
Mchezaji huyo ambaye ni kinara kwa ufungaji akipachika mabao tisa mpaka sasa ameeleza ligi ya msimu huu ni ngumu ukilinganisha na msimu uliopita hivyo amezitaka timu shiriki ziendelee kupambana ili kuifanya ligi hiyo izidi kuwa bora.