Riyadh, Saudi Arabia
Karim Benzema amesaini mkataba wa miaka mitatu kuichezea klabu ya Al-Ittihad ya Saudi Arabia ikiwa ni takriban siku tatu baada ya kuaga katika klabu ya Real Madrid.
Benzema ambaye ni mshindi wa Ballon d’Or, ametwaa mataji 25 hadi sasa yakiwamo matano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, manne ya La Liga na hadi anaondoka Real Madrid alikuwa mshambuliaji tegemeo wa timu hiyo.
Mchezaji huyo pia anashika nafasi ya pili kwa kuifungia Real Madrid mabao mengi akiwa amefikisha mabao 354 akizidiwa na Cristiano Ronaldo aliyefikisha mabao 450. Ronaldo naye kwa sasa yuko Saudi Arabia akiichezea klabu ya Al Nassr.
“Ni ligi nzuri na ina wachezaji wengi wazuri, Cristiano Ronaldo tayari yuko, ni rafiki na hiyo inaonyesha kwamba Saudi Arabia imeanza kupiga hatua, niko hapa kwa ajili ya kushinda kama nilivyofanya nikiwa Ulaya,” alisema Benzema.
“Nimekuwa mwenye bahati kwa kufanikisha mambo mazuri katika maisha yangu ya soka na kufanikisha kila kitu nilichoweza nikiwa Hispania na Ulaya, hatimaye nimeona ni wakati sahihi wa kuikimbilia changamoto mpya,” alisema Benzema.
Klabu ya Al-Ittihad kwa sasa inanolewa na kocha wa zamani wa klabu za Wolves na Tottenham, Nuno Espirito Santo.
Mchezaji mwingine ambaye anahusishwa na mipango ya kwenda kucheza soka Saudi Arabia ni Lionel Messi ambaye anatakiwa na klabu ya Al Hilal ingawa klabu yake ya zamani ya Barcelona nayo inamtaka.