Madrid, Hispania
Real Madrid hatimaye imekamilisha usajili wa kiungo wa England, Jude Bellingham kutoka klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani kwa ada ya Pauni 88.5 milioni na mkataba wa miaka sita.
Habari zaidi zinadai kwamba kwa ujumla mkataba wa Bellingham unaweza kufikia Pauni 115 milioni ukijumuisha na makubaliano mengine ya ziada.
Bellingham ambaye ana umri wa miaka 19 alianza kuwindwa na vigogo hao wa Hispania mara baada ya fainali za Kombe la Dunia, anatarajia kutangazwa rasmi katika hafla maalum kesho Alhamisi.
Kwa muda wote ambao amekuwa na Dortmund, Bellingham amekuwa akisifika kwa umahiri wake katika nafasi ya kiungo na Oktoba mwaka jana aliweka rekodi ya kuwa nahodha wa kwanza mwenye umri mdogo katika timu hiyo akiwa na miaka 19.
Nyota huyo wa zamani wa Birmingham City, baada ya kukamilisha usajili huo aliwashukuru Dortmund kuanzia mashabiki na kila mmoja kwa yote mazuri katika kipindi cha miaka yake yote na timu hiyo.
“Ni heshima kubwa kuvaa jezi ya timu yenu mara nyingi katika matukio makubwa na madogo na ingawa najiandaa kwenda hatua nyingine sitosahau safari yangu pale, nawatakia kila la heri kwa mambo yajayo,” alisema Bellingham.
Kwa usajili huo, Bellingham anaingia katika orodha ya wachezaji wa bei mbaya waliosajiliwa na timu hiyo lakini anakuwa mchezaji wa pili ghali wa England baada ya Jack Grealish ambaye Man City ilimsajili mwaka 2021 kutoka Aston Villa kwa ada ya Pauni 100 milioni.