Vancouver, Canada
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limetangaza kuwa wanachama wake 54 wanamuunga mkono rais wa sasa wa Fifa, Gianni Infantno katika uchaguzi wa shirikisho hilo.
Kauli ya kumuunga mkono Infantino imetolewa na Rais wa CAF, Patrice Motsepe (pichani) ambaye amekuwa na ukaribu wa kikazi na kiongozi huyo wa Fifa, ukaribu ambao umekuwa na manufaa kwa bara la Afrika.
Infantino, 56, alikabidhiwa majukumu ya kuongoza Fifa mara ya kwanza mwaka 2016 akichukua nafasi ya mkongwe Sepp Blatter na sasa anajiandaa kwa uchaguzi uliopangwa kufanyika mwaka 2027 na kama atashinda ataongoza kwa kipindi kingine cha miaka minne.
Mapema mwezi huu, Shirikisho la Vyama vya Soka Marekani Kusini (CONMEBAL) walikuwa wa kwanza kutangaza kumuunga mkono Infantino ambaye hata hivyo bado hajatangaza nia ya kuwania kuongoza Fifa kwa kipindi kingine cha miaka minne.
Katika chaguzi mbili zilizopita za Fifa za mwaka 2019 na 2023, Infantino alipita bila kupata mpinzani na tangu wakati huo hadi sasa amefanya mabadiliko makubwa katika mchezo huo unaopendwa zaidi duniani.
Kura 54 za Afrika zinawakilisha robo ya kura zote 211 kutoka vyama vya soka vya nchi mbalimbali duniani na ni dhahiri kwamba kura hizo za Afrika zina mchango mkubwa katika ushindi wa Infantino.
Infantino amekuwa akiungwa mkono Afrika hasa baada ya kuongeza misaada kupitia programu ya Fifa Forward lakini pia ameongeza ushiriki wa Afrika kwenye fainali za Kombe la Dunia pamoja na kutoa kipaumbele kwa bara hilo katika uwekezaji wa maendeleo kwenye miradi ya soka.
Kimataifa CAF kumpa kura Infantino Fifa
CAF kumpa kura Infantino Fifa
Read also
