Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi, amewapongeza wachezaji wake kwa kucheza kwa kujituma, kujitolea na kufanikiwa kupata pointi tatu ambazo zimeendelea kuwaweka ndani ya malengo yao msimu huu.
Yanga ilivuna ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ihefu jana kwenye mechi ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam na kuifanya miamba hiyo kufikisha pointi 53 na kuzidi kujikita kileleni mwa msimamo.
Kocha huyo ameeleza kuwa pamoja na ugumu waliokutana nao kutoka kwa Ihefu, lakini siri kubwa inayowasaidia kupata ushindi katika kila mchezo ni kuwaheshimu wapinzani na kuzungumza mara kwa mara na wachezaji wake juu ya umuhimu wa kuendelea kupata matokeo.
“Tumekutana na timu ngumu ambayo ilijiandaa vizuri kuliko sisi na hiyo ilitokana na kuchelewa kuanza mazoezi kutoka kwenye mapumziko mafupi na kuchanganya wachezaji wapya na wale waliokuwepo lakini nafurahi kuona walicheza kwa juhudi na kupata pointi tatu ambacho ndio kilikuwa kitu muhimu zaidi kwetu.
“Tulichelewa kupata bao na ushindi ni kutokana na uchezaji wa wapinzani wetu katika kukaba kuanzia juu na ni kitu ambacho kiliwanyima utulivu wachezaji wangu awali na kushindwa kufanya maamuzi ya haraka, hivyo nawapongeza kwa hilo,” alisema Nabi.
Naye kocha msaidizi wa Ihefu, Zuber Katwila ameeleza kuwa waliingia kwenye mchezo huo lengo likiwa kupata pointi moja au zote tatu lakini mambo yalikuwa tofauti baada ya kipa wao kufanya kosa ambalo liliwapa wapinzani wao bao la ushindi.
“Pamoja na kupoteza lakini wachezaji wamefuata kwa asilimia kubwa yale tuliyokusudia na siwezi kumlaumu kipa wetu kwa kosa alilolifanya sababu kabla ya hapo ameokoa hatari nyingi zaidi ya kosa alilofanya pengine tungeweza kufungwa idadi kubwa zaidi ya hilo moja,” alisema Katwila.
Soka Nabi awapongeza wachezaji Yanga
Nabi awapongeza wachezaji Yanga
Related posts
Read also