London, England
Mwamuzi msaidizi wa Ligi Kuu England (EPL) Constantine Hatzidakis hatochukuliwa hatua za kinidhamu baada ya kumuomba radhi beki wa Liverpool, Andy Robertson aliyedaiwa kumpiga kiwiko.
Hatzidakis alidaiwa kumpiga kiwiko Robertson Jumapili iliyopita katika mechi kati ya Arsenal na Liverpool iliyopigwa kwenye dimba la Anfield na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Chama cha Soka England (FA) kilitarajiwa kumpa adhabu mwamuzi huyo ambaye ilidaiwa kwamba alimpiga kiwiko mchezaji huyo baada ya wawili hao kuzozana.
Tukio hilo lilitokea wakati wa mapumziko ambapo Robertson alimkusa mkononi mwamuzi huyo ambaye alijibu mapigo kwa kumpiga beki huyo wa kushoto sehemu ya usoni akitumia kiwiko.
Hata hivyo baada ya uchunguzi wa siku nne kwa kutumia video na taarifa kutoka kwa waamuzi, wachezaji na mashahidi wengine, FA ilithibitisha kwamba Hatzidakis hatopewa adhabu.
“Tumepitia ushahidi wote unaohusisha tukio zima lililotokea Anfield likimhusisha beki wa Liverpool, Andrew Robertson na mwamuzi Constantine Hatzidakis na hatutochukua hatua zozote,” alisema msemaji wa FA.
Inadaiwa kwamba jana Alhamisi Hatzidakis mwenyewe alimuomba radhi Robertson kwa tukio hilo na Robertson alikubali na kumsamehe bila kusita.
“Haikuwa dhamira yangu kumgusa Andy kwa namna yoyote wakati nikiuondoa mkono wangu karibu naye na kwa hilo namuomba msamaha. Kwa sasa najiandaa kuendelea na kazi yangu ya kusimamia mechi za soka,” alisema mwamuzi huyo.
