Na mwandishi wetu
Mzimu wa sare unaendelea kuisumbua Yanga katika Ligi Kuu NBC baada ya kujikuta ikipata matokeo ya sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar katika mechi iliyochezwa Jumamosi Machi 21, 2026 kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Katika mechi hiyo iliyojaa ushindani licha hali ya uwanja kuathiriwa na mvua za hapa na pale, Yanga ndio waliokuwa wa kwanza kuzitikisa nyavu za Mtibwa katika dakika ya 24 kwa bao lililofungwa na Pacome Zouzoua.
Baada ya bao hilo, Yanga waliendelea kuutawala mchezo kwa kusaka bao la pili huku wakidhibiti kasi ya wachezaji wa Mtibwa waliokuwa wakihaha kusaka bao la kusawazisha.
Juhudi za Mtibwa zilizaa matunda dakika za nyongeza (dk 90+2) walipopata bao lililofungwa na Ismail Mhesa, bao lililozua tafrani kwa wachezaji wa Yanga wakiongozwa na kipa wao, Djigui Diarra kumzonga mwamuzi wa mechi hiyo.
Yanga hata hivyo itabidi wajilaumu kwa kushindwa kuzitumia nafasi kadhaa walizozipata ambazo zingeweza kuwafanya watoke uwanjani na pointi tatu badala ya moja.
Matokeo hayo yamezidisha hasira za mashabiki wa Yanga na sasa wameanza kuusakama uongozi hasa kwenye mitandao ya kijamii, wengine wakitaka kocha Pedro Concalves atimuliwe huku wengine wakimtetea.
Hii inakuwa sare ya nne kwa Yanga katika mechi za karibuni, ilianza kupata matokeo ya aina hiyo dhidi ya hasimu wake Simba timu hizo zilipomaliza dakika 90 bila kufungana, ikafuatiwa na sare nyingine mbili dhidi ya Azam FC na baadaye TRA United.
Yanga hata hivyo inaendelea kuushikilia usukani wa ligi hiyo ikiwa kileleni na pointi 38 baada ya kucheza mechi 16 ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 29 ikiwa imecheza mechi 15 na Simba ni ya tatu ikiwa na pointi 28 katika mechi 13.
Soka Sare zageuka kero Yanga
Sare zageuka kero Yanga
Related posts
Read also
