Manchester, England
Man City leo Jumanne itaumana na Real Madrid katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, mechi ambayo inatarajiwa pia kutawaliwa na mpambano baina ya mshambuliaji wa Man City, Erling Haaland na beki wa Real Madrid, Antonio Rudiger.
Rudiger alipata heshima akidaiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kumdhibiti Haaland katika mechi ya kwanza ya nusu fainali msimu uliopita ambayo iliisha kwa sare ya bao 1-1 kabla ya City kushinda kwa mabao 4-0 katika mechi ya marudiano.
Wakati mashabiki wakiwaza uwezekano wa kuwapo mpambano kati ya Rudiger na Haaland, kocha wa City, Pep Guardiola yeye anaamini wapinzani wao wataingia uwanjani kwa lengo la kulipa kisasi.
Kauli ya Pep inatokana na kumbukumbu ya matokeo ya mechi ya msimu uliopita yaliyoifanya City kusonga mbele hadi hatua ya fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-1 na hatimaye kubeba taji.
“Ni ngumu jambo hilo kujirudia mara ya pili, kuifunga Real Madrid mara mbili mfululizo ni jambo lisilowezekana, wamejifunza kitu na watataka kulipa kisasi, wana kitu cha kujivunia,” alisema Pep.
Kwa upande wake, Rudiger, beki wa zamani wa Chelsea alizungumzia jinsi walivyomdhibiti Haaland katika mechi ya kwanza ingawa alikosa nafasi katika mechi ya marudiano ambayo timu yake ilifungwa.
Akizungumzia hali ilivyokuwa katika mechi ya kwanza, Rudiger alisema mechi ilikuwa nzuri na walifanikiwa kumdhibiti Haaland kupewa pasi za kuzalisha mabao.
“Kocha hakuniomba radhi kwa kutonipa nafasi (mechi ya pili) na hahitaji kufanya hivyo, nalikubali hilo ingawa ni ngumu kulipokea, na sasa mpango wetu katika mechi hii ni kuwadhibiti wachezaji hatari kama Phil Foden, De Bruyne, na ipo wazi kwamba mwingine ni Haaland,” alisema Rudiger.
Rudiger pia alimsifia kiungo wao Jude Bellingham ambaye hakuwapo katika mechi iliyopita akisema kwamba atawaongeza nguvu kubwa katika timu yao kwenye mechi dhidi ya City.
“Awali nilishangaa sikuwa nikimjua sana, lakini acha tu jamaa yuko sawa, anakubalika hadi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, namna alivyo makini na mambo yake ni jambo zuri, ndio kwanza ana miaka 20 lakini ana mambo makubwa, kuna siku ataiongoza (timu ya taifa) England,” alisema Rudiger.
Mechi za leo Jumanne Ligi ya Mabingwa Ulaya
Arsenal v Bayern Munich
Real Madrid v Man City