Na mwandishi wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewapongeza wanamichezo wote waliofanya vizuri katika mashindano ya kimataifa ikiwamo timu ya Taifa ya wasichana chini ya miaka 17 ya Serengeti Girls.
Pongezi hizo zilitolewa na Rais Samia leo Ikulu jijini Dar es Salaam alipowaalika wachezaji wa Serengeti Girls na viongozi wao kula nao chakula cha mchana na kusema kuwa anafarijika kuona timu ya wanawake imekuwa ya kwanza kufuzu fainali za soka za Kombe la Dunia kabla ya wanaume.
Serengeti Girls ni timu ya kwanza kufuzu fainali za soka za Kombe la Dunia kwa Tanzania ukiacha ile ya walemavu na sasa inajiandaa kushiriki fainali za michuano hiyo zitakazofanyika nchini India kuanzia Oktoba 11 hadi 30 mwaka huu.
Timu hiyo imefuzu ikiwa na rekodi nzuri ya ushindi mfano imeibugiza Botswana juma ya mabao 11-0 baada ya ushindi wa mechi mbili za nyumbani na ugenini kisha kuifunga Burundi kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-2 kabla ya kumalizia kazi kwa ushindi dhidi ya Cameroon na kukata tiketi ya fainali hizo.
Serengeti katika fainali hizo wanaungana na timu za Nigeria na Morocco ambao ni wawakilishi kutoka Afrika, timu nyingine shiriki ni pamoja na wenyeji India, Mexico, Ufaransa, Colombia, Japan, Chile, Canada, China, Marekani, Brazil, New Zealand, Ujerumani na Hispania.
Serengeti katika fainali hizo imepangwa Kundi D na timu za Japan, Canada na Ufaransa wakati wenyeji India wapo Kundi A na timu za Brazil, Marekani na Morocco. Kundi B lina timu za New Zealand, Chile, Ujerumani na Nigeria na Kundi C lina timu za China, Colombia, Mexico na Hispania.
