i

Na mwandishi wetu
Mabao matatu ya DR Congo yameiwezesha timu hiyo kutoka kifua mbele kwa ushindi wa 3-0 dhidi ya Taifa Stars katika mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2022 dhidi ya Taifa Stars.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Stars iliuanza mchezo kwa kasi na kuisumbua DR Congo ambao katika kipindi cha kwanza walicheza wakionekana kama wanausoma mchezo wa Stars.
Pamoja na Stars kuanza kwa kasi lakini walikuwa ni DRC waliofanya shambulizi la maana na kupata bao katika dakika ya tano lililofungwa na nyota wa klabu ya Lens ya Ufaransa, Gael Kakota aliyefumua shuti lililomshinda kipa Aishi Manula.
Bao hilo halikuwatoa mchezoni Stars kwani wakiongozwa na nahodha wao, Mbwana Samatta na Simon Msuva waliendelea kuisumbua ngome ya DRC lakini hadi mapumziko DRC walikuwa mbele kwa bao hilo moja.
Juhudi za Stars kusaka bao zilikatishwa tamaa katika dakika ya 65 baada ya Idumba Fasika anayekipiga Afrika Kusini katika klabu Cape Town City kuandika bao la pili ambalo lilizidi kupoteza matumaini ya Stars kutoka nyumbani na ushindi.
Katika hali ambayo haikutarajiwa, Stars ambayo katika mechi ya kwanza na DRC ugenini ilitoka sare ya bao 1-1 ilijikuta ikilala kwa bao la tatu katika dakika ya 85 lililofungwa na Ben Maiango anayeichezea Raja Casablanca ya Morocco.
Kuingia kwa bao hilo kulionekana kuwachanganya hadi mashabiki ambao baadhi walianza kutoka nje ya uwanja huku DRC ambao sasa wanaongoza kundi J wakiwa na pointi nane wakicheza taratibu na kupoteza muda.
Stars inabaki na pointi zake saba wakati mechi nyingine ya kundi hilo itachezwa baadaye leo kati ya Benin na Madagascar.
Katika mechi nyingine ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia, mahasimu wa Afrika Mashariki, Kenya na Uganda waliumana na kutoka sare ya bao 1-1.
