Na mwandishi wetu
Nahodha wa Simba, John Bocco amewaomba mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuwaunga mkono kipindi hiki ambacho timu yao inapitia wakati mgumu wa kukosa matokeo.
Simba haijapata ushindi katika michezo mitatu mfululizo, kati ya hiyo miwili ni ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya AC na Raja Casablanca kabla ya jana Jumanne kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam kwenye Ligi Kuu NBC.
Bocco alikiri mambo kuwa magumu kwao lakini kingine kinachosababisha hilo ni uchovu uliotokana na kucheza mechi ngumu bila kupata muda wa kupumzika.
“Tunaomba mashabiki wetu watuvumilie, ni matokeo mabaya ambayo hatujayatarajia lakini hizi ni nyakati ambazo timu yoyote inaweza kuikuta lakini naamini yatapita na timu itarudi kwenye uwezo wake uliozoeleka,” alisema Bocco.
Mshambuliaji huyo ameeleza kuwa matokeo wanayoyapata hata yeye na wachezaji wenzake hawafurahishwi nayo lakini wanajitahidi kupambana kuepuka mwenendo huo mbaya kwenye mashindano yote.
Kuhusu ubingwa, nahodha huyo alisema bado wana nafasi ya kubeba taji hilo la ligi msimu huu ingawa wanalazimika kushinda mechi zao saba zilizobaki na kuwaombea mabaya watani zao Yanga kwenye mechi zilizosalia.