London, England
Uteuzi wa beki wa kati wa Man United, Harry Maguire katika kikosi cha England umemuibua kocha wa Crystal Palace, Patrick Vieira ambaye amesema kwamba beki huyo amekosewa heshima na waandishi wa habari.
Maguire amekuwa mjadala kwa muda mrefu sasa akilaumiwa kwa kucheza chini ya kiwango na hata kutokuwa na uhakika wa namba katika kikosi cha kwanza cha Man United akiwa amecheza mechi tisa tu msimu huu hali iliyoibua hofu kwamba kocha wa England, Gareth Southgate huenda asingempa nafasi kwenye kikosi cha timu hiyo kitakachokwenda Qatar kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Southgate hata hivyo juzi alimtaja mchezaji huyo katika kikosi cha wachezaji 26 na baada ya uteuzi huo Vieira ameibuka na kusema, “Maguire ni mchezaji wa kiwango cha juu na mwenye kujiamini, kuna wakati unaweza kucheza vizuri na kuna wakati unacheza vibaya lakini hilo haliondoi sifa alizonazo na tabia zake binafsi za kibinadamu. Taifa la England litafaidika kutoka kwake.”
Viera aliongeza, “nafikiri kuna wakati nyinyi (vyombo vya habari) hamkuonyesha kumheshimu Maguire na kwa baadhi ya wachezaji ambao wamechaguliwa kwenye timu ya Taifa.”
Katika uteuzi wa kikosi cha England, Southgate hakumpa nafasi beki wa Crystal Palace, Marc Guehi, ambaye aliitwa kwenye timu hiyo kwa mara ya kwanza Machi mwaka huu katika mechi dhidi ya Switzerland iliyopigwa kwenye dimba la Wembley.
Kuhusu beki wake huyo Vieira alisema, “Marc anachotakiwa kufanya ni kuwa juu wakati wote katika kiwango chake, kama utamlinganisha Marc na Maguire hao ni wachezaji wawili tofauti, Maguire anajua mambo ya kiwango cha kimataifa ambayo Marc bado hajayajua.
“Kocha anatakiwa kufanya maamuzi kuhusu nini anahitaji katika mashindano hayo, Marc au mtu mwingine yeyote anatakiwa kuheshimu uamuzi huo na kutoa hukumu mara baada ya mashindano, kocha anawajua vizuri wachezaji wake kuliko sisi, anajua nini anahitaji kwa wachezaji na vipi atawatumia katika staili ya uchezaji,” alisema Vieira.
Kimataifa Waandishi wamemkosea heshima Maguire-Vieira
Waandishi wamemkosea heshima Maguire-Vieira
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
