Na mwandishi wetu
Ushindi mdogo wa bao 1-0 dhidi ya KMC umekuwa na maana kubwa kwa Yanga baada ya kuzidi kuipaisha katika mbio zake za kulitetea taji la Ligi Kuu NBC msimu huu wa 2022/23.
Clement Mzize (pichani) ndiye aliyeifanya Yanga kutoka kifua mbele kwa bao la dakika ya 38 akiutumia mpira wa kona uliopigwa na Dickson Ambundo kabla ya kuokolewa na kipa wa KMC, David Kissu.
Kwa ushindi huo Yanga imeendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa imefikisha pointi 62 na kuwaacha mahasimu wao Simba wanaoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi nane.
Ili wafanikiwe kulitetea taji hilo, Yanga sasa ina kazi ya kusubiri mechi tano zijazo ili ishinde zote na kufikisha pointi 77 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote kwenye ligi.
Ushindi huo mbali na kuipaisha Yanga kwenye mbio za kulitetea taji, pia umekuja dhidi ya timu ambayo imekuwa ikiwapa upinzani kama alivyozungumza kabla ya mechi hiyo kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze.
Kaze alinukuliwa na GreenSports akisema kwamba KMC wamekuwa wapinzani wakubwa kwao na kutarajia mechi kutokuwa rahisi.
Baada ya ushindi huo, Yanga sasa inajiandaa kwa ajili ya mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Real Bamako ya Mali, mechi itakayopigwa Februari 26 wakati siku moja kabla Simba itaumana na Vipers ya Uganda katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Soka Yanga yazidi kupaa
Yanga yazidi kupaa
Read also