Real Madrid wataka majibu Uefa
Madrid, Hispania
Baada ya kuilaza Liverpool bao 1-0 na kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Real Madrid imetaka majibu kuhusu matukio ya uvunjifu wa amani wakati wa mechi ya fainali baina ya timu hizo.
Real Madrid na Livcrpool ziliumana, Mei 28 mwaka huu jijini Paris, Ufaransa katika mechi ya fainali ya ligi hiyo, mechi ambayo kabla ya kuanza ilitawaliwa na matukio ya uvunjifu wa amani na kusababisha mechi kuchelewa kuanza zaidi ya nusu saa huku polisi wakiwatawanya mashabiki kwa mabomu.
Klabu hiyo pia imetaka kujua sababu za kuuchagua Stade de France jijini Paris kwa ajili ya mechi hiyo hasa baada ya wenye mamlaka kuwatelekeza mashabiki. Uamuzi wa mechi hiyo kuchezwa Stade de France badala ya St Petersburg mjini Zenit, Urusi ulichukuliwa baada ya Urusi kuivamia Ukraine na hivyo mechi hiyo kuzuiwa kuchezwa katika nchi hiyo.
Katika tukio la kabla ya mechi hiyo, mashabiki wengi wanaodaiwa kuwa wa Liverpool ndio waliojikuta katika wakati mgumu kuingia uwanjani huku wengi wao wakidaiwa kuwa na tiketi feki jambo ambalo inadaiwa ndio chanzo kimojawapo cha vurugu.
Real Madrid katika taarifa yao wameeleza kusikitishwa na matukio hayo wakidai kuwa hali iliyokuwa katika maeneo ya kuingilia Stade de France na hata ndani ya uwanja hayakuwa mazuri na mashabiki wao walijikuta wakiwa wahanga.
“Tungependa kujua sababu zilizotumika kuchagua uwanja huo (Stade de France) kuwa mwenyeji wa mechi ya fainali na vigezo husika kwa kuzingatia tukio lililotokea siku ya mechi,” ilifafanua taarifa hiyo.
Zaidi ya hilo, taarifa hiyo ya Real Madrid pia ilitaka majibu na maelezo ya kina ili kujua wahusika waliowaacha mashabiki katika hali ya kutelekezwa, mashabiki ambao Real Madrid wanadai kuwa wamekuwa mfano mzuri kila wakati.
Wakati yote hayo yakiendelea, Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) tayari limeunda kamati maalum huru itakayoandaa ripoti kuhusu tukio hilo.
