Na mwandishi wetu
Mwenyekiti wa Bodi ya Simba SC, Salim Abdallah ‘Try Again’ amewaomba Watanzania wote kuisapoti Simba katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi ya Soka Afrika’(AFL) dhidi ya Al Ahly ya Misri kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam keshokutwa Ijumaa.
Akizungumza Dar es Salaam leo Jumatano, Try Again (pichani juu) alisema mechi hiyo si ya Simba pekee bali ya Watanzania wote na kuhimiza umuhimu wao wa kushiriki kwa wingi.
“Hii ni mechi ya Watanzania sio Simba. Niwaombe Watanzania waje kwa wingi. Simba inawakilisha Watanzania kwenye michuano hii kwa hiyo watu wanunue tiketi mapema, hii michuano ni mipya na Tanzania imepata nafasi ya kuandaa mechi ya kwanza hivyo ni heshima kwa taifa zima,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema wamefanya maandalizi mazuri mfano wa michuano ya Kombe la Dunia na anaamini kila shabiki atakayeenda uwanjani atafurahia kwa kila kitu.
Kuhusu maandalizi ya timu, alisema wako kambini wanaendelea vizuri na kwamba asilimia kubwa ya wachezaji waliokwenda kuwakilisha timu zao za Taifa wamerejea na wako tayari kwa mapambano.
Alisema anaamini Simba ni timu ya kiwango cha juu na inaweza kufanya makubwa hasa linapokuja suala la kimataifa wanakuwa hawana huruma hivyo, watu wategemee ushindi mkubwa katika mchezo dhidi ya Al Ahly.
“Mpira utakaochezwa ni ule unaopita kwenye njia zake, ikiwezekana Ahly atakufa nyingi. Bado sisi tupo kwenye kiwango cha juu,”alisema na kuongeza kuwa anawashukuru Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) Gianni Infatino na wa Afrika (Caf) Patrice Motsepe kwa kuwapa heshima hiyo ya kipekee,” alisema Try Again.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan naye ameahidi kutoa zawadi ya Sh milioni 10 kwa kila bao litakalofungwa na Wekundu hao katika michuano hiyo.
Wakati huo huo Try Again pia alisema kwamba Rais wa heshima na mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji ameandaa fungu la bonasi kwa wachezaji ikiwa watafanya vizuri katika mchezo huo.