Na mwandishi wetu
Mratibu wa pambano la ngumi kati ya Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ na Erick Katompa wa DR Congo, Meja Seleman Semunyu amesema mambo yameiva na mabondia wote wawili wako kamili.
Katika pambano hilo la raundi 10 na lisilo la ubingwa, Dulla Mbabe (pichani) atakuwa na kibarua cha kulipa kisasi baada ya kushindwa kutamba kwa Katompa walipokutana mara ta mwisho.
Kwa mujibu wa Semunyu, pambano hilo linatarajiwa kuchezwa Julai 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kinesi, Sinza, Dar es Salaam na kuhusisha jumla ya mapambano 10 ya ndani na kimataifa.
Semunyu alisema mabondia wote wanaendelea na maandalizi vizuri na anaamini litakuwa pambano lenye msisimko kutokana na kila mmoja kutaka kuonesha yeye ni bora kuliko mwenzake kwa sasa.
“Dulla Mbabe anataka kulipa kisasi na kudhihirisha kuwa kipigo cha kwanza kilikuwa cha kubahatisha na Katompa atataka kuonesha ushindi wake wa mwanzo ulikuwa sahihi, pambano litakuwa la msisimko,” alisema.
Alisema katika kuhakikisha pambano hilo linakuwa na hadhi ya kimataifa tayari ameutengeneza uwanja wa Kinesi kwa kuweka taa zaidi ya 50 na kuhakikisha mazingira ya milango ya kuingilia yanakuwa bora na salama kwa ulinzi kwa watakaokuja kushuhudia.
Alitaja viingilio vya pambano hilo kuwa ni kuanzia Sh 7,000 kwa waliokata tiketi mapema, Sh 10,000 mlangoni na 20,000 kwa VIP.
Mara ya mwisho mabondia hao walikutana mwaka 2021, Dulla Mbabe alipoteza pambano hilo kwa pointi 94-93, 97-90 na 94-93.
Ngumi Dulla Mbabe kulipa kisasi kwa Katompa?
Dulla Mbabe kulipa kisasi kwa Katompa?
Read also