Na mwandishi wetu
Timu ya Al Ahly ya Misti imeendelea kujiimatrisha kileleni mwa msimamo wa Kundi B katika Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Yanga katika mechi iliyochezwa Jumamosi Januari 31, 2026 kwenye Uwanja wa Amaan,Zanzibar.
Matokeo hayo yanazidi kuiweka Yanga pagumu katika mkakati wake wa kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo kwani wakati Ahly ikishika usukani wa kundi hilo na pointi, Yanga inabaki na pointi tano.
Timu nyingine zilizo Kundi B ni AS FAR Rabat ya Morocco na JS Kablie ya Algeria ambazo zilicheza siku hiyo hiyo na AS Rabat kupata ushindi wa bao 1-0 hivyo kufikisha pointi tano kama za Yanga.
Ili kufufua matumaini ya kusonga mbele Yanga itabidi ipambane kufa na kupona ili kupata ushindi katika mechi yake ijayo ya ugenini dhidi ya AS Rabat itakayochezwa Februari 7, 2026.
Ikishangiliwa na mashabiki wake waliofurika kwenye Uwanja wa Amaan, Yanga ilikuwa ya kwanza kuzitingisha nyavu za Ahly kwa bao la Ibrahim Bacca dakika chache kabla ya timu kwenda mapumziko.
Bao hilo lilitokana na makosa ya safu ya ulinzi ya Ahly kujichanganya wakati Yanga ikilisakama lango lao na mpira kumkuta Bacca ambaye alifumua shuti lililomshinda kipa, Mostafa Shobeir na kujaa wavuni.
Kipindi cha pili, Ahly walionesha utulivu wakimiliki mpira na kutanua uwanja kwa pasi huku wakitengeneza mashambulizi kadhaa langoni mwa Yanga ambao walikuwa na kazi ya kujihami zaidi kuliko kushambulia.
Mashambulizi hayo ya Ahly yalionekana kumkera zaidi kipa wa Yanga, Djigui Diarra ambaye mara kadhaa alionekana akiwalaumu mabeki wake.
Katika dakika ya 60 ndipo Ahly walipotengeneza shambulizi lililozaa bao lililotokana na kona iliyopigwa na Ahmed Mostafa kabla ya mpira kumkuta Mahmoud Hassan ‘Trezeguet’ aliyemsogezea Alliou Dieng ambaye aliujaza mpira wavuni.
Katika mechi ya mwisho baina ya timu hizo, Yanga ikiwa ugenini ililala kwa mabao 2-0, mfungaji wa mabao hayo akiwa ni Trezeguet.
Kimataifa Yanga, Al Ahly zatoka sare
Yanga, Al Ahly zatoka sare
Read also
