Manchester, England
Mshambuliaji majeruhi wa Man United, Benjamin Sesko atazikosa mechi muhimu za kufuzu Kombe la Dunia na timu yake ya taifa ya Slovenia huku pia kukiwa na hatihati kuhusu kuwa fiti na kuiwakilisha vyema United.
Sesko aliumia Jumamosi iliyopita katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Tottenham iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2 na hivyo kuibua habari kwamba ameumia sana na mbali na timu ya taifa pia atakosa mechi kadhaa za Man United.
Baada ya kucheza kwa dakika 30 kwenye mechi na Tottenham, Sesko alitoka uwanjani huku akichechemea baada ya kuumia goti alipokuwa akikabiliana na Micky van de Ven.
Sesko aliyesajiliwa Man United kwa Pauni 73.7 milioni alionekana akiwa amekaa chini ya uwanja na ingawa muda mfupi baadaye aliinuka lakini utokaji wake uwanjani ulikuwa katika namna iliyotia shaka.
Alipoulizwa kuhusu Sesko, kocha wa Man United, Ruben Amorim alisema kwa sababu ni tatizo la goti ni vigumu kujua hivyo atafanyiwa vipimo na suala hilo huenda likaathiri mipango ya usajili wa mchezaji huyo wakati wa dirisha dogo la Januari.

Kuna hofu kubwa kwamba huenda mchezaji huyo akaongeza idadi ya wachezaji watakaokosekana katika kikosi cha Man United wakiwamo washambuliaji Bryan Mbeumo na Amad Diallo na beki Noussair Mazraoui.
Wahezaji hao watatu mwezi Desemba watakuwa na timu zao za taifa kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) itakayofanyika nchini Morocco.
Kwa upande wa timu ya taifa ni wazi kwamba Sesko atazikosa mechi mbili muhimu za timu hiyo dhidi ya Kosovo na Sweden, mechi ambazo watahitaji kushinda ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu Kombe la Dunia kupitia play offs.
