Na mwandishi wetu
Kiungo mpya wa Yanga, Mudathir Yahya ameeleza kuwa ana jukumu kubwa la kuonesha thamani yake ndani ya kikosi cha Yanga baada ya kupewa nafasi ya kuitumikia timu hiyo kipindi hiki.
Mudathir ambaye amesajiliwa juzi na Yanga, alieleza usajili huo umekuwa kama bahati kwake kwani hakuwa akilifikiria hilo kwa kipindi chote cha nusu msimu alichokaa bila timu tangu alipoachana na Azam mwishoni mwa msimu uliopita.
“Kwanza nimshukuru Mungu kupata nafasi hii ya kusajiliwa na Yanga, nilikuwa nafanya mazoezi tu nyumbani lakini ikatokea bahati ya kusajliwa na Yanga, nikasajiliwa,” alisema Mudathir.
“Nafahamu kuwa kuna ushindani mkubwa kikosini, nimewakuta kwenye nafasi zao na ninajua nina jukumu kubwa la kuonesha uwezo wangu maana hata kocha anajua umuhimu ndiyo maana nimesajiliwa hivyo nahitajika kuonesha kitu na kupata nafasi,” alisema.
Kiungo huyo ambaye juzi alijiunga na timu hiyo visiwani Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi amesisitiza kuwa yupo tayari kwa ajili ya mechi za ushindani kwani muda mrefu amekuwa akijifua vilivyo licha ya kutokuwa na timu.
Aidha, mchezaji huyo wa zamani wa Singida United ujio wake umetafsiriwa kama kuja kuziba nafasi ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyetengaza kuvunja mkataba na klabu hiyo hivi karibuni licha ya suala lake kuendelea kutafutiwa ufumbuzi.
Mudathir sasa ataungana na viungo wengine kuwania nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo wakiwemo Khalid Aucho, Yanick Bangala, Gael Bigirimana, Zawadi Mauya na Salum Aboubakary ‘Sureboy’.
Soka Mudathir kuonyesha thamani Yanga
Mudathir kuonyesha thamani Yanga
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
