Na mwandishi wetu
Baada ya kuwapo uvumi kuhusu Kelvin Nashon kutua Simba, hatimaye klabu hyo imemtangaza rasmi kiungo huyo kuwa mchezaji wao mpya atakayeitumikia timu hiyo kuanzia msimu mpya wa 2026-27.
Taarifa hiyo rasmi imepatikana leo Jumapili Julai 19, 2026 kwenye mitandao ya kijamii ya klabu hiyo ikiambatana na picha ya kumkaribisha kiungo huyo fundi kutoka Pamba Jiji.
Habari za Kelvin kujiunga na Simba zimekuwapo kwa miezi kadhaa lakini hazikuwa zimethibitishwa na klabu hiyo na hivyo sasa ni rasmi kuanzia msimu ujao nyota huyo ambaye pia amewahi kuichezea Singida Black Stars atavaa jezi ya Simba.
Habari za Simba kumtaka kiungo huyo ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, zilianza kusikika wakati akiwa Singida Black Stars kabla ya kwenda Pamba Jiji, Januari 2025.
Simba ambayo imemaliza Ligi Kuu NBC msimu ulioisha wa 2025-26 ikiwa nafasi ya pili, inaendelea kuimarisha kikosi chake ikiacha baadhi ya wachezaji na kusajili wapya kwa ajili ya msimu mpya wa ligi hiyo na michuano ya kimataifa.
Azam, Yanga nazo zasajili
Wakati Simba ikikamilisha usajili huo Azam FC nao wameendelea kukiimarisha kikosi chao kwa kumsajili winga Henoc Nolia kutoka FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mitadao ya Azam kuanzia Jumamosi Julai 18, 2026 imepambwa na picha za mchezaji huyo mpya ambaye ataongeza nguvu katika kikosi cha timu hiyo iliyomaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu NBC msimu wa 2025-26.
Nao mabingwa watetezi wa Ligi Kuu NBC, Yanga wametangaza kumsajili mshambuliaji Juma Issa Abushiri maarufu Chuga Boy kutoka Fountain Gate FC.
Chuga ndiye mchezaji wa kwanza kutambulishwa na Yanga kwa ajili ya kukiongezea nguvu kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya msimu mpya wa 2026-27.
Kimataifa Kelvin Nashon rasmi mali ya Simba
Kelvin Nashon rasmi mali ya Simba
Read also
