Na mwandishi wetu
Uongozi wa Coastal Union umeeleza kuwa mpaka sasa umepokea wasifu wa makocha zaidi ya 50 kwa ajili ya kurithi nafasi ya Mwinyi Zahera (pichani) aliyepewa jukumu jipya la Mkurugenzi wa Ufundi wa Coastal.
Ofisa Habari wa Coastal, Abbas El-Sabri amesema leo Jumanne kuwa kwa sasa uongozi unaendelea kuyapitia maombi hayo kabla ya kumchagua mmoja kuwa kocha mkuu wa timu hiyo yenye maskani yake Tanga.
“Zahera tulimbadilishia majukumu na kwa sasa ni mkurugenzi wa ufundi pamoja na msimamizi wa timu zetu za vijana chini ya miaka 17 na 20. Kuhusu kocha mkuu uongozi ndio unalishughulikia hilo, naamini ndani ya siku chache zijazo tutamtangaza kocha mpya na watu watamjua,” alisema El Sabri.
Alisema pamoja na kuanza msimu vibaya malengo yao msimu huu ni kuhakikisha wanamaliza ligi katika nafasi za juu huku wakitaka kucheza fainali ya michuano ya Kombe la FA (ASFC).
Kiongozi huyo alisema wana uhakika wa kutimiza malengo yao na hiyo ni kutokana na ubora wa kikosi walichokisajili msimu huu akiwemo nahodha wao, Ibrahim Ajibu.
Uongozi wa mabingwa hao wa ligi mwaka 1988, uliamua kumweka pembeni Zahera kutokana na matokeo mabaya waliyoyapata kwenye mechi za mwanzoni za ligi ambazo zimewafanya washike nafasi ya 14 wakikusanya pointi sita katika mechi saba walizocheza.