Na mwandishi wetu
Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars imeibuka na ushindi wa kishindo kwa kuichapa timu ya Macau mabao 6-0 katika mwendelezo wa mechi maalum za Fifa (Fifa Series) mjini Kigali, Rwanda.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumapili Machi 29, 2026, Stars ilitawala kwa kiwango kikubwa mchezo huo baada ya kushindwa kutamba katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Liechtenstein ilipolala kwa bao 1-0.
Ukurasa wa mabao ya Stars ulianza kufunguliwa dakika ya 15 ya mchezo kwa bao la kuzawadiwa baada ya Amancio kujifunga katika harakati za kuokooa na dakika 10 baadaye, Bakari Mwamnyeto akaiongezea Stars bao la pili.
Mudathir Yahya aliongeza bao la tatu kwa Stars muda mfupi kabla ya timu kwenda mapumziko na hivyo kufanya timu zende mapumziko, Stars wakiwa mbele kwa mabao 3-0.
Kipindi cha pili Stars iliendeleza moto wake na kuandika bao la nne dakika ya 56 lililofungwa na Paul Peter wakati bao la tano lilifungwa na Novatus Dismas dakika ya 74 na Allarakhia akakamilisha idadi ya mabao sita dakika tatu kabla ya mpira kumalizika.
Hii ni mechi ya sita kwa kocha Miguel Gamondi tangu akabidhiwe jukumu la kuinoa timu hiyo siku chache kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon 2025) zilizofanyika kuanzia Desemba mwaka jana nchini Morocco.
Chini ya Gamondi, Stars imecheza mechi nne za Afcon 2025 na kuishia hatua ya 16 bora kabla ya kutolewa na wenyeji Morocco na mechi nyingine mbili za michuano ya Fifa Series.
Kimataifa Stars yapata ushindi wa kishindo
Stars yapata ushindi wa kishindo
Read also
