Na mwandishi wetu
Simba leo Jumapili imeifuata Yanga kwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Power Dynamos ya Zambia na hivyo kuneemeka na mabao ya ugenini.
Timu hizo mbili zilitoka sare ya mabao 2-2 katika mechi ya kwanza iliyopigwa Ndola Zambia na sasa Simba inasubiri kujua timu pinzani katika hatua hiyo baadaye mwezi huu.
Katika mechi ya leo iliyopigwa kwenye dimba la Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam, Dynamos ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 16 mfungaji akiwa ni Andy Boyeli ambaye alionesha juhudi binafsi za kumiliki mpira kabla ya kufumua shuti lililojaa wavuni.
Simba ilianza kusaka bao la kusawazisha na dakika 10 baada ya kuanza kipindi cha pili, nahodha John Bocco aliyeingia kuchukua nafasi ya Jean Baleke, akiwa katika nafasi nzuri aliinasa pasi ya Clatous Chota Chama na kufumua shuti lililotoka nje ya lango. Kosakosa hiyo ilionekana kuwakera mashabiki wa Simba waliojawa na hofu ya timu yao kutolewa huku baadhi yao wakianza zomeazomea za hapa na pale na wengine kuonekana kutokubaliana na uamuzi wa kocha kumuingiza Bocco.
Bocco hata hivyo aliwajibu mashabiki hao katika dakika ya 69 kwa kupiga krosi ambayo beki wa Dynamos, Kondwani Chiboni alijikuta akiipa Simba bao la kusawazisha wakati akijaribu kuokoa mpira huo.
Bao hilo lilionekana kuwatuliza mashabiki ambao baadhi yao walionekana kujawa hofu wakihisi jahazi lilikuwa likielekea kuzama na Bocco baada ya juhudi hizo alionekana kama kuwatuliza mashabiki hao kwa ishara.
Simba pamoja na kufuzu hatua hiyo baadhi ya mashabiki hawakufurahia namna timu yao ilivyocheza na kwa muda mwingi wa mchezo walionekana kujawa hofu na wengine kutoridhika kwa timu yao kufuzu kwa faida ya mabao ya ugenini.
Mahasimu wao Simba, Yanga jana nao walifuzu hatua hiyo hiyo baada ya kuitoa Al Merrikh ya Sudan kwa kuichapa bao 1-0 na hivyo kufuzu kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-0 baada ya ushindi wa mechi ya kwanza wa mabao 2-0 ambao ulipatikana Yanga ikiwa ugenini.
Wakati huo huo wawakilishi wengine wa Tanzania, Singida Fountain Gate wameshindwa kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya leo kulala ugenini kwa mabao 4-0 mbele ya Future ya Misri.
Singida wanakuwa wametolewa kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya kwanza ambayo Singida walikuwa wenyeji.
Kimataifa Simba yaifuata Yanga makundi Afrika
Simba yaifuata Yanga makundi Afrika
Read also