Manchester, England
Kocha wa Man City, Pep Guardiola amesema timu yake inakabiliwa na janga la wachezaji wengi majeruhi hali ambayo inaweza kuathiri mwanzo mzuri waliouanza msimu huu.
Man City jana Jumanne iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Red Star Belgrade lakini pamoja na ushindi huo wachezaji majeruhi wanamtia hofu Pep.
Mafanikio yao katika mechi saba za mashindano yote yamechangiwa na kiungo Bernardo Silva ambaye naye ameingia katika orodha ya majeruhi na kwa mujibu wa Pep, atakosekana uwanjani wiki kadhaa.
Silva katika orodha hiyo anaungana na kina John Stones, Jack Grealish, Kevin de Bruyne pamoja na Mateo Kovacic ambao wote ni majeruhi.
Hali hiyo imejitokeza baada ya hivi karibuni timu hiyo kuwapiga bei, Riyad Mahrez, Cole Palmer na Aymeric Laporte huku aliyekuwa nahodha wao Ilkay Gundogan akihamia Barcelona baada ya kumaliza mkataba wakati Joao Cancelo, Tommy Doyle na James McAtee wakiuzwa kwa mkopo.
Man City inajiandaa kwa mechi tatu ngumu zilizo mbele yake ikiwamo ya Oktoba 8 dhidi ya Arsenal katika Ligi Kuu England na kufuatiwa na mechi ya Carabao dhidi ya Newcastle na mechi nyingine ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya RB Leipzig kabla ya mapumziko.
Mazingira yote hayo yanamfanya Pep kuamini kwamba timu yake ipo katika wakati mgumu hali ambayo imewakuta wakiwa wametoka kuweka historia kwa kubeba mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi Kuu England na FA msimu uliopita.
“Tuko katika majanga lakini sisemi aah tuna majeruhi, hapana japo hiyo ndiyo hali hali, kwa wachezaji tulionao tutapambana kitu cha muhimu ni kuwa na fikra sahihi, hilo ndilo jambo zuri,” alisema Pep.